Na.Lina Sanga
Kilele cha maadhimisho ya kwanza ya siku ya kiswahili duniani leo Julai 7, 2022 uwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa utakuwa na matukio makubwa matatu, yatakayofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa,Balozi Profesa Kennedy Gastorn ameieleza Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa,kuwa tukio la kwanza litakuwa asubuhi kuanzia saa 4 kwenye ukumbi namba 3 wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, likihusisha hotuba kutoka kwa viongozi wa ngazi ya juu akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Marais na wakuu wa nchi zinazozungumza lugha ya Kiswahili.
“Viongozi wakuu wa nchi watatoa matamko yao akiwemo Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Marais kutoka kusini mwa Afrika kama Msumbiji na Zimbabwe, tunatarajia viongozi wa Afrika Mashariki mfano Uganda na Kenya na viongozi wa mashirika makubwa kama Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO,” amesema Balozi Gastorn.
Amesema baada ya matamko ni wakati wa mjadala utakaojikita katika nafasi ya Kiswahili katika amani ya maendeleo, Wazungumzaji ni pamoja na wanazuoni, watu binafsi, sekta binafsi na viongozi wa Serikali.
Aidha amesema kuwa licha ya mjadala huo pia watatoa maoni yao ni kwa vipi kiswahili kimekuwa ni nyenzo ya kuendeleza amani, kuunganisha watu na katika kuendeleza maisha ya watu tunapoelekea kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu "SDGS.”
"UN imepitisha azimio la matumizi ya lugha mbalimbali 'multilingualism' na lugha ya Kiswahili ni miongoni mwao,"amesema Profesa Kennedy.
Sehemu ya tatu ni maonesho ya mila na desturi za kiswahili ikiwemo mavazi, chakula na nyimbo na hili litafanyika kwenye ofisi za uwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.
“Cha kutia moyo ni kwamba kutakuwepo na watoto wa shule ya awali kutoka hapa Marekani ambao wanajifunza lugha ya kiswahili ,Wataonesha umahiri wao katika kiswahili na hili ni jambo la furaha kama wanavyosema wahenga kuwa ‘ngoma inayodumu ni ile inayochezwa na marika yote’ hivyo uwepo wa watoto wa shule ya awali nje ya mipaka ya Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika ni ishara nzuri kwamba kweli sasa kiswahili kinashika hatamu,” amesema Balozi Gastorn.
Ametanabaisha kuwa kwa mara ya kwanza mkutano na mjadala ndani ya Umoja wa Mataifa,utaendeshwa kwa lugha ya kiswahili kwa sababu kutakuwepo na wakalimani wa lugha zote rasmi za Umoja wa Mataifa kutoka lugha ya Kiswahili.
#jiandaekuhesabiwa2022
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa