Na. Lina Sanga
Njombe
Mikataba ya lishe itayotumika kwa miaka nane imesainiwa leo Mkoani Njombe,kati ya Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya,Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji na Wilaya.
Akiwasilisha taarifa ya utiaji saini mikataba hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Dkt. Zabron Masatu katika kikao cha utiaji saini mikataba ya lishe kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe,ambapo amebainisha kuwa Mkoa wa Njombe una asilimia 53.6 ya watoto wenye udumavu.
Amesema kuwa katika mikataba hiyo iliyosainiwa leo kuna kazi kuu mbili ambapo kazi ya kwanza ni afua ya lishe na ili kuweza kusimamia afua mbalimbali za lishe mikataba ni muhimu ili kuhakikisha wananchi hasa watoto walio chini ya miaka mitano wanapata lishe.
Dkt. Masatu amesema kuwa,moja ya afua ambazo zimekuwa zikisimamiwa sana ni kuweka mipango mizuri ya lishe kwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato ya ndani, kulingana na idadi ya watoto wanaopatikana katika Halmashauri au Mkoa husika. ambapo kila mtoto mmoja anatengewa shilingi 1,000 kwa kila robo mwaka.
“Mfano Mkoa wa Njombe tuna watoto 110,000 kwa iyo kwenye afua hii ya lishe kila mtoto inatakiwa atengewe si chini ya shilingi 1,000 na tumekuwa tukitenga fedha hizo,jambo kubwa ambalo tunatakiwa kulisimamia ni upatikanaji wa fedha hizo na matumizi yake,kwa mwaka uliopita tulifanikiwa kwa asilimia 78 na kwa mwaka huu tunahitaji kujipanga vizuri ili tufikie asilimia 100,kwa sababu haya ni maelekezo ya Serikali na zaidi ya hilo tunahitaji kuhakikisha afya za watoto wetu hasa walio chini ya miaka mitano zinaimarika kwa ajili ya ustawi wa uchumi wan chi yetu”,alisema Dkt. Masatu.
Pia,amebainisha kuwa katika afua za afya kuna afua ya utoaji wa matone ya vitamini A kwa watoto chini ya miaka mitano na vidonge vya kuongeza damu kwa kina mama wajawazito,kwani endapo mama mjamzito ana afya sio nzuri na ana damu pungufu hata mtoto atayezaliwa atakuwa hana afya nzuri na huenda ikapelekea mama huyo kutojifungua salama na kupata matatizo hata kifo.
Aidha,Dkt. Masatu Amesema kupitia mikataba ya lishe iliyosainiwa leo,kuna afua ya watoto wanaopata chakula shuleni kupata chakula chenye vitamini,na Serikali imeanza kufanya majadiliano na wadau mbalimbali katika sekta ya biashara kuhakikisha kwenye halmashauri zote kuna wasagaji wa chakula ambao watakuwa na uwezo wa kusaga mahindi au vyakula mbalimbali na kuweka virutubisho kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi.
Judica Omari,Katibu Tawala Mkoa wa Njombe ametoa agizo kwa wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha fedha hizo za lishe kwa ajili ya watoto zinatengwa katika bajeti kwa kila robo,na zinapatikana lakini pia amewataka Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi kuhakikisha vikao vya lishe vinafanyika kwa kuzingatia ratiba kwani ni vikao vya kisheria.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa