Na. Lina Sanga
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa amezindua zoezi la utoaji wa hatimiliki kwa wananchi wa Mtaa wa Sekondari,Kata ya Maguvani baada ya zoezi la urasimishaji ardhi kupitia mradi wa MKURABITA kukamilika.
Kabla ya kutoa hati hizo Mhe. Kissa ameshukuru na kupongeza mradi wa MKURABITA kwa kuona umuhimu wa utekelezaji wa mradi huo katika Wilaya ya Njombe hususani Halmashauri ya Mji Makambako.
Amesema kuwa anatambua Halmashauri nyingi, Kata na Mitaa mingi inahitaji mradi kama huo,hivyo wananchi ambao hawajakamilisha malipo ya hati wakamilishe malipo ili zoezi la umilikishwaji likamilike.
Ametoa msisitizo kwa wananchi ambao maeneo yamefanyiwa urasimishaji na kumilikishwa ardhi kutumia hati hizo kwa manufaa,kwa kutumia vizuri mikopo watayochukuwa kupitia hati hizo kwa kufanyia malengo na sio kuongeza idadi ya ndoa.
Ametoa wito kwa taasisi za fedha kutoa elimu ya mikopo kwa wananchi ili wapate manufaa kupitia mikopo wanayopata,kwa kuwajengea uelewa juu ya mikopo.
Lakini pia amemuomba Mratibu wa MKURABITA Taifa,kumaliza kazi ya urasimishaji wa ardhi kwa maeneo yaliyobaki,kama alivyoahidi kukamilisha zoezi hilo baada ya fedha kupatikana.
“Nikuombe Mratibu wa MKURABITA Taifa, kumaliza kazi ya urasimishaji wa ardhi kwa maeneo yaliyobaki kama ulivyoahidi,mimi kwa kushirikiana na Mkurugenzi pamoja na viongozi wa Mtaa na Chama kuwahimiza wananchi kufanya nafasi yao na MKURABITA wafanye nafasi yao ili zoezi la urasimishaji likamilike.
Mhe. Kissa ametoa rai kwa wananchi wa Mtaa huo kukamilisha malipo ya umilikishwaji ili wananchi wa Mtaa wa Kikula pia,wanufaike kupitia mradi huo kwani MKURABITA hawawezi kuanza urasimishaji Kikula kabla ya kukamilisha zoezi katika Mtaa wa Sekondari.
Ametoa wito kwa wananchi wote kujiandaa kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na Makazi kuanzia usiku wa kuamkia Agosti 23,kwa kuandaa taarifa zote muhimu kwa ajili ya Sensa pamoja na kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa wataofika katika kaya zao kwa kutoa taarifa za kweli kwa manufaa kwa umma.
Pia ametoa wito kwa wakulima kujiandikisha kwa ajili ya kupata mbolea yenye ruzuku kwenye maeneo wanayolima,ili wanufaike na mbolea hiyo na sio kwenye maeneo wanayoishi.
Lakini pia ametoa wito na angalizo kwa watendaji wasio waaminifu wanaodai fedha kwa ajili ya uandikishaji wa wakulima kuacha mara moja,kwani hakuna gharama yoyote ya uandikishaji.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa