Na. Tanessa Lyimo
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe.Kissa Gwakisa Kasongwa leo amekabidhi hundi yenye thamani ya Mil. 474.9 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri ya Mji Makambako.
Mhe.Kissa akizungumza na wanufaika hao katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ukumbi wa kanisa la Romani Katoliki la Ilangamoto, amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuwa waaminifu wakati wa urejeshaji, ili iweze kuwanufaisha walengwa wengine wanaohitaji mikopo na ameipongeza Halmashauri ya Mji Makambako pamoja na madiwani kwa kusimamia na kuhakikisha fedha zilizotolewa kwa dhumuni la mikopo ya asilimia kumi inatolewa kwa walengwa na kutotumika kwa matumizi mengine.
Naye, mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako Mhe. Hanana Mfikwa ametoa rai kwa wanufaika kutumia mikopo hiyo katika malengo yaliyokusudiwa na sio vinginevyo, ili kuepuka usumbufu wakati wa urejeshaji wa mikopo hiyo.
Bw.Khamis Shemababu wa kikundi cha “The Fighters” kutoka Kata ya Mjimwema, katika Mtaa wa Bwawani kwa niaba ya wanufaika wote ameishukuru Serikali kwa mikopo hiyo huku akitoa wito kwa vijana kuwa na tabia ya kujishughulisha kwani kwa kupitia uwajibikaji na mikopo inayotolewa na Halmashauri itawawezesha wao kuendesha maisha yao na kunufaika kiuchumi.
Halmashauri ya Mji makambako ilipokea jumla ya maombi 157 katika vikundi mbalimbali yenye thamani ya Bil 2.5 na kwa awamu ya kwanza ya utoaji wa mikopo hiyo Halmashauri imeweza kukopesha jumla ya vikundi 81 vilivyokidhi vigezo kiasi cha Mil.474.9 , vikundi vya wanawake 57 , vijana 14 na kundi la watu wenye ulemavu 10
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa