Na. Lina Sanga
Njombe
Wilaya ya Njombe kwa kipindi cha miaka mitatu imepata hasara ya moto ulioteketeza jumla ya hekta 16,980.6 za misitu yenye thamani ya zaidi ya Bil. 316 katika Halmashauri ya Mji Njombe,Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Halmashauri ya Mji Makambako.
Taarifa hiyo imetolewa na Mhifadhi wa Misitu Mwandamizi wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS)Wilaya ya Njombe,Audatus Kashamakula katika kikao kazi cha Mkuu wa Mkoa wa Njombe na Wahe. Madiwani,Wakurugenzi wa Halmashauri,Wakuu wa idara na Vitengo,Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji,Watendaji wa Kata,Mitaa na Vijiji wa Halmashauri zilizopo Wilaya ya Njombe,kikao hicho kimefanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Kashamakula amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020/2021 hadi oktoba 2022/2023 Wilaya ya Njombe imepata matukio 51 ya moto ulioteketeza hekta nyingi za misitu ambapo chanzo kikubwa ni Uchomaji wa mkaa, uchomaji wa mashamba ya miti kwa makusudi ili kuwakomesha wamiliki wa mashamba hayo ikiwa kuna migogoro ya familia na kusababisha hasara kwenye mashamba yaliyo jirani.
Amesema kuwa wananchi wengi wa Njombe wana utamaduni wa kizamani wa kuandaa mashamba kwa kuchoma moto pasipokuwa na mikakati mizuri ya kudhibiti moto na kusababisha ajali za moto ambao unateketeza rasilimali nyingi za misitu na moto mwingi unaanzia kwenye maeneo ambayo wawekezaji wanatumia wafanyakazi kutoka nje ya Mkoa wa Njombe ikiwemo kupasua mbao na kusababisha moto wanapoandaa chakula.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka amekemea vikali tabia ya baadhi ya watu wanaochoma mashamba ya watu kwa makusudi ili kulipiza kisasi kwani wanawapa hasara na wengine wasiohusika na ugomvi wao na kusababisha janga katika uchumi wa Mkoa mzima.
Katika matukio hayo ya moto katika Wilaya ya Njombe,Halmashauri ya Mji Makambako kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 imepata hasara ya moto ulioteketeza jumla ya hekta 23.6 zenye thamani ya Mil. 440.5,mwaka 2021/2022 jumla ya hekta 11.4 zenye thamani ya Mil. 212.8 ziliteketea kwa moto na mwaka 2022/2023 kuanzia mwezi julai hadi oktoba jumla ya hekta 14.6 zenye thamani ya Mil. 272.5 zimeteketea kwa moto.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa