Na. Lina Sanga
Dodoma
Bil. 9.5 kukamilisha mradi wa ujenzi wa soko la wazi la machinga complex (Samia open machinga complex),unaojengwa Bahi road Halmashauri ya Jiji Dodoma.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji Dodoma,Iglco Nicodemous katika ziara ya Maafisa habari wa Mikoa,Halmashauri na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI Jijini Dodoma.
Mhandisi Nicodemous amesema kuwa soko hilo la wazi lenye ukubwa wa mita za mraba 15,000, lina uwezo wa kutosha machinga 3,150 lengo kuu ni kuwakusanya machinga wote katika eneo moja na kuwakutanisha na wateja wao na kufanya biashara kivulini.
Amesema kuwa machinga 3,150 wametambuliwa na timu ya uratibu iliyoundwa kwa kushirikiana na machinga wenyewe kupitia uongozi wao,hivyo si rahisi mtu mwingine kuingia sokoni baada ya utambuzi huo na vigezo vya utambulisho wa machinga kilizingatiwa.
Nicodemous ameongeza kuwa baada ya ujenzi kukamilika,machinga waliotambuliwa watakabidhiwa vizimba vya kufanyia biashara bure bila malipo,machinga watalipia huduma mbalimbali ambazo zitakuwa zikitolewa eneo la soko kama usafi na choo.
"Machinga hawatalipia gharama za vizimba bali watalipia huduma kama usafi wa soko na huduma ya choo,watoa huduma kama benki na mama lishe watachangia gharama za upangaji ", alisema Nicodemous.
Chanzo cha fedha za ujenzi wa mradi huo ni mapato ya ndani pamoja na fedha za mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya Uviko 19 mil.500 na bil 2.5 zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Maafisa habari pia wamepata nafasi ya kutembelea Mji wa Serikali "Mtumba" ambao miradi ya ujenzi wa majengo ya ofisi mbalimbali za Serikali inatekelezwa,pamoja na miradi miwili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa 51.2 KM yenye thamani ya bil 89 na barabara yenye urefu wa 20KM inayotekelezwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA).
Ziara hiyo ni moja kati ya agizo la Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wa Ofisi Rais TAMISEMI alilolitoa jana kwa Katibu Mkuu wakati wa kikao cha Maafisa habari wa Mikoa, Halmashauri na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI,ili Maafisa habari waweze kutembele miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika Jiji la Dodoma ,ikiwa ni moja ya azimio kuu la vikao vya Maafisa habari kutembelea miradi katika maeneo ambayo kikao kinafanyika.
#jiandaekuhesabiwa2022
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa