Na.Lina Sanga
Sensa ni utaratibu wa kukusanya,kuzichambua na kuzichakata taarifa za watu katika maeneo husika kwa kutambua umri wao,viwango vyao vya elimu,shughuli zao za kiuchumi na kijamii ambazo zinafanyika ili zisaidie Serikali,katika kuandaa Sera na Mipango ya maendeleo na kufanya tathimini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ambayo imewekwa.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Sensa Halmashauri ya Mji Makambako,Ingbert Kindimba katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika kijiji cha Kifumbe na Usetule,Kata ya Mahongole ikiwa ni sehemu ya Ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa ya Kijiji kwa Kijiji,Mtaa kwa Mtaa katika Halmashauri ya Mji Makambako.
Kindimba amesema kuwa Sensa ya watu hufanyika kila siku katika ngazi ya familia,mama anapoandaa chakula huzingatia idadi ya watu katika kaya yake vivyo hivyo katika taifa letu,Halmashauri yetu na Vijiji vyetu ili tuweze kuandaa mipango ya maendeleo jambo la kwanza ni kupata idadi sahihi ya watu ndipo mipango iandaliwe.
Amesema kuwa mgawanyo wa pato la taifa kigezo kikuu ni idadi ya watu katika taifa,Ujenzi wa madarasa,vituo vya Afya,Zahanati na mahitaji ya dawa huzingatia idadi ya watu katika vijiji,mitaa,Kata,Mji hadi Mkoa,na idadi ya watu inapatikana kupitia zoezi la Sensa hivyo usipohesabiwa utakwamisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika eneo lako unaloishi.
Kindimba amesema kuwa Zoezi la Sensa litaanza rasmi usiku wa agosti 22 kuamkia siku ya Sensa agosti 23 hadi agosti 28 mwaka huu kwa kuzingatia mahali alipolala mtu huyo,Usiku wa kuamkia tarehe ya Sensa na taarifa za watu wote katika kaya zitatolewa na mkuu wa kaya ambaye anaaminiwa na wana kaya wengine anaweza kuwa baba,mama au mtoto wa familia husika.
“Mkuu wa Kaya sio lazima awe baba wa familia,anaweza kuwa mama au mtoto wa familia hiyo ambaye anaaminiwa na wanakaya wengine kuwa anaweza kutoa taarifa sahihi kuhusu wana kaya wengine,hivyo kwa mwanaume ambaye ana mke zaidi ya mmoja atahesabiwa alipolala usiku wa kuamkia siku ya Sensa agosti 23,kaya zingine mkuu wa kaya atakuwa mke na sio mume tena,wasafiri na watu wengine wasio na makazi maalumu watahesabiwa usiku wa kuamkia Siku ya Sensa katika maeneo walipolala inaweza kuwa nyumba za kulala wageni,vituo vya mabasi,vituo vya treni na maeneo ya masoko ambako watoto wanaoishi mitaani wanalala”,alisema Kindimba.
Ametoa wito kwa wanawake ambao wameolewa na mume mwenye mke zaidi ya mmoja kujenga uaminifu katika utoaji wa taarifa,endapo mwanaume alilala kwa mke mwingine asihesabiwe tena kwani kila mtu atahesabiwa mara moja tu,ili takwimu sahihi za watu zipatikane kwa maendeleo ya taifa,endapo taarifa zitakazotolewa hazitakuwa sahihi,athari zake kwa taifa ni za miaka kumi kwani Sensa inafanyika kila baada ya Miaka kumi hivyo mipango ya maendeleo haitaweza kutekelezwa ipasabyo.
Mwisho amewataka wananachi wote kujiandaa kuhesabiwa na kuwa tayari kutoa taarifa sahihi,kwani taarifa zote zinazotolewa ni za siri Karani atayehusika na kukusanya taarifa za watu na makazi yao,ataongozana na wajumbe wa Serikali za vijiji au Mitaa yao,kila mwana kaya ana haki ya kuhesabiwa awe mlemavu wa viungo au akili wote watahesabiwa mara moja tu.
#jiandaekuhesabiwa2022
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa