Ofisi ya Rais ikulu kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) imeiwezesha halmashauri ya Mji Makambako kutekeleza mradi wa urasimishaji viwanja na nyumba katika mitaa miwili ambayo ni mtaa wa Kikula katika Kata ya Makambako na mtaa wa Sekondari katika Kata ya Maguvani.
Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa Urasimishaji Mijini,Mwesige Ileta alipokuwa akiutambulisha mradi huo kwa Viongozi wa mitaa ambayo itanufaika na mradi huo katika halmashauri ya Mji Makambako.
Mwesige amesema kuwa mradi huo wa urasimishaji katika halmashauri ya Mji Makambako utafanyika katika mitaa miwili,ambayo ni mtaa wa kikula na mtaa wa sekondari ili kuwasaidia wananchi wote kuwa na hatimiliki.
Amesema kuwa lengo kuu la Serikali ni kuwapunguzia mzigo wananchi kwa kuwalipia gharama za upangaji na upimaji wa nyumba na viwanja,ili mwananchi ashughulike na ulipaji wa gharama za hatimiliki pekee,tofauti na sasa ambapo mwananchi anatakiwa kulipia gharama za upangaji,upimaji na hatimiliki.
Mwesige ameongeza kuwa zoezi hilo la urasimishaji linalotarajiwa kuanza hivi karibuni,litafanyika sambamba na utoaji wa hatimiliki kwa viwanja visivyopungua elfu moja kwa watu waliolipia tu.
"Gharama za urasimishaji wa viwanja na nyumba kwa sasa ni laki moja na elfu thelathini, ambayo ni gharama ya upangaji na upimaji wa viwanja pekee, baada ya hapo inatakiwa mtu alipie gharama za hatimiliki ya kiwanja sasa ili kumpunguzia mwananchi kulipa gharama mara mbili,Ofisi ya Rais kupitia mradi wa MKURABITA imeamua kulipia gharama za upimaji na upangaji ili mwananchi alipie gharama za hatimiliki ambayo ni gharama ya mwisho",alisema Mwesige.
Amewaota hofu wananchi ambao tayari walishafanya malipo ya urasimishaji kuwa fedha zao zipo salama na zitatumika kulipia hatimiliki,na zitazobaki watarejeshewa kupitia watendaji wa mitaa ambao ndiyo wasimamizi wa akaunti hizo kwa kushirikiana na kamati za urasimishaji za mitaa husika kwani huenda gharama zitapungua.
Aidha Mwesige amesema kuwa gharama za umilikishaji zinatofautiana kati ya kiwanja kimoja na kingine,kutokana na ukubwa au matumizi ya kiwanja husika kama ni makazi na biashara,makazi au biashara pekee.
Ametoa Wito kwa wananchi wa mtaa wa Kikula na Sekondari kuchangamkia fursa hiyo,kwani haitajirudia na wananchi wengi wanaihitaji hivyo kila mwananchi ambaye ana kiwanja au nyumba,katika mitaa hiyo ni vema kufanya malipo kupitia akaunti za urasimishaji za mitaa yao baada ya kupewa bili wakati wa zoezi la upangaji na upimaji,ili wanufaike na mradi huo kwani hatimiliki ina faida nyingi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa