Na. Lina Sanga
Njombe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan ameupongeza Mkoa wa Njombe kwa ukusanyaji Mzuri wa mapato kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na, kuwapongeza Wakurugenzi kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwataka kuendelea kuongeza juhudi katika ukusanyaji aa mapato ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mhe. Samia ametoa pongezi hizo leo alipokuwa akihutubia wananchi wa Mkoa wa Njombe leo,katika Viwanja vya sabasaba ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe.
Kuhusu ombi la Viongozi la Mkoa wa Njombe kupandishwa hadhi kuwa Manispaa,Mhe. Samia amesema kuwa kutokana na hali ya uchumi kwa sasa ugawaji wa maeneo mapya ya kiutawala au kupandisha hadhi,umezuiliwa na muelekeo ni kwa wananchi,mapinduzi ya kilimo na kunyanyua hali ya uchumi kabla ya kugawanya maeneo ya utawala.
Ameongeza kuwa kuhusu ombi la ujenzi wa chuo kikuu katika Mkoa wa Njombe, kuna mradi wa ujenzi wa vyuo vikuu ambao unaruhusu vyuo kuweka matawi katika Mikoa,hivyo endapo kuna nafasi ya ujenzi wa chuo kikuu chochote,tawi litajengwa Njombe na endapo mradi umebana ameahidi kulifanyia kazi kwa wakati mwingine ili kupitia mradi huo tawi la chuo kikuu lijengwe Mkoani Njombe.
Pia, amesema kuwa kujenga mazingira ya kuwezesha kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla,miradi na mazingira ya uwekezaji inayowekwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya nchini ,hawana budi kubeba na kutekeleza kwa moyo mkunjufu kwani miradi mingine hujenga fursa za watanzania kufanya miradi na shughuli zao za maendeleo,kujipatia kipato na kulipandisha taifa kwani kujenga uchumi wa taifa unaanza chini kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Ametoa wito kwa Viongozi na wananchi kuchapa kazi, kwani mazingira yanayojengwa na ruzuku zinazotolewa ni kwa ajili ya kufanya kazi na kuzalisha kwa tija na kwa wingi,na kuuza kwa wingi ili kupata mapato ya kutosha na kujenga taifa.
Kuhusu utawala bora,Mhe. Samia suluhu ametoa rai kwa viongozi wote kuanzia ngazi ya chini hadi Mkoa kuhudumia na kutumikia wananchi,kwani viongozi sio watawala bali wahudumu.
"Niwaombeni twendeni tukahudumie wananchi tumewekwa na Mungu ametuteuwa tuwahudumie wananchi kwa utawala bora,kama umebahatika kukaa hapo ulipokaa mwananchi akija muhudumie vizuri kwani wananchi hawana shida,tunapowaomba kura tunatoa ahadi nyingi sana tunapopata kura tunawageuka, twende tuwahudumie wananchi",amesema Mhe. Samia.
Mwisho ametoa wito kwa watanzania wote kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya watu na Makazi, inayotarajiwa kuanza agosti 23, mwaka huu kwa mipango endelevu ya nchi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa