Na. Lina Sanga
Njombe
Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa Wakala wa barabara Vijijini (TARURA),kulinda hadhi ya taasisi hiyo kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya matengenezo ya barabara ili kuto sababisha kero kwa wananchi.
Mhe. Mtaka ametoa wito huo leo katika kikao cha utiaji saini mikataba ya matengenezo na ukarabati wa barabara na ujenzi wa madaraja, kwa mwaka wa fedha 2022/2023,kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Amesema kuna baadhi ya wakandarasi ni wazembe na hawatekelezi kazi zao kwa wakati na kusababisha kero kwa wananchi wanaotumia barabara hizo,kama kumwaga kifusi bila kukisambaza kwa muda mrefu.
Mhe. Mtaka amesema kuwa endapo kuna Mkandarasi hana uhakika na uwezo wake wa kazi ni vema asisaini mkataba wa kuanza kazi,kwani endapo akishindwa kukamilisha mradi ndani ya muda uliopangwa sheria itachukua mkondo wake,kwani baadhi ya wakandarasi wabovu wanasababisha ofisi na viongozi kutukanwa kwa kazi mbovu wanazofanya.
“Mkandarasi akiharibu kazi anasababisha ofisi na viongozi kutukanwa kwa uzembe wao,watu wanaanza kusema amepewa kazi na Mkuu wa Mkoa mara amepewa kazi na kiongozi wa ofisi Fulani, lakini kumbe kila mkandarasi ameomba kazi mwenyewe na endapo kama kuna mkandarasi amepata kazi kwa kupewa na mtu Fulani aseme au ametoa rushwa ndiyo amepata kazi ajitokeze ili asijehukumiwa pindi atakapoharibu kazi”.alisema Mhe. Mtaka.
Ametoa angalizo kwa wakandarasi wote kutumia fedha watakazolipwa kukamilisha kazi,kwani endapo mradi hautakamilika kwa uzembe hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Jumla ya mikataba 22 yenye thamani ya zaidi ya Bil. 22 imesainiwa leo mbele ya Mkuu wa Mkoa,Katibu Tawala Mkoa,Wakuu wa Wilaya,Makatibu Tawala wa Wilaya,Wakurugenzi,Kamati za Usalama,Viongozi wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya na Mkoa,Viongozi wa dini pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa