Na. Lina Sanga
Njombe
Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka amemuagiza Afisa elimu wa Mkoa wa Njombe kuweka utaratibu wa kuwaandaa wanafunzi wanaoingia madarasa ya mitihani mapema baada ya kumaliza mitahala ya mwaka husika na kuwapa walimu uhuru wa kutekeleza jambo hilo ifikapo mwaka 2023 kama shule binafsi zinavyofanya ili kuongeza ufaulu katika Mkoa wa Njombe.
Mhe. Mtaka ametoa agizo hilo leo katika kikao maalumu na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne wa shule za Sekondari za Serikali zilizopo katika Halmashauri ya Mji Makambako wanaotarajia kuanza mitihani ya kuhitimu masomo ya sekondari novemba 14 mwaka huu.
Amesema kuwa Shule za Serikali kuanzia Msingi hadi Sekondari zinaendeshwa kimazoea bila mitazamo chanya yenye manufaa kwa wanafunzi kwa walimu kukosa uhuru wa kubuni mbinu mbalimbali kukuza taaluma.
“Shule binafsi kwa muda ambao wanafunzi wa darasa la nne wamemaliza mtihani wa taifa,wanawaandaa wanafunzi wa darasa la tatu kwa kuwafundisha masomo ya darasa la nne,wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaoingia kidato cha pili mwakani wameshaanza mitahala ya kidato cha kwanza lakini wanafunzi wa shule za Serikali ambao wamemaliza mitahala ya mwaka huu wanaenda tu shuleni kutimiza wajibu hadi shule zitapofunga na hawana maandalizi yoyote ya masomo ya mwaka ujao na tunategemea kutokomeza sifuri kivipi?”, alisema Mhe. Mtaka.
Aidha amemtaka Afisa elimu wa Mkoa kuhakikisha idadi ya walimu kufika makao makuu ya Halmashauri kufuata huduma inapungua kwa Maafisa waliopo ofisi kuu kuwafuata walimu kwenye vituo vyao vya kazi kwa kutumia magari ya Serikali na walimu waendelee na jukumu la kufundisha.
Ametoa wito kwa wanafunzi wote wa kidato cha nne kufanya mitihani yao vizuri na kutambua Mhe. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafanya jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu ya shule na kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaofaulu vizuri.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa