Na. Lina Sanga
Njombe
Waziri wa Uwekezaji,Biashara na Viwanda, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa rai kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha sheria ndogo za Halmashauri zinazotungwa , kwa ajili ya usimamizi wa masuala mbalimbali ya kiutendaji hazipingani na sheria kubwa zilizopo ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Dkt. Ashatu ametoa rai hiyo leo katika mkutano wa saba wa baraza la biashara, Mkoa wa Njombe lililofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe ,baada ya kuibuka kwa malalamiko ya wafanyabiashara wa mbao kutozwa ushuru wa mbao shilingi 100 hadi 200 kwa ubao badala ya asilimia 3.
Amesema kuwa,sheria kubwa inamtaka mfanyabiashara kulipa ushuru wa mbao asilimia 3 lakini baadhi ya Halmashauri zinaendelea kumtoza mfanyabiashara shilingi 100 kwa kila ubao, ambapo ni kinyume cha sheria na ni kikwazo kwa wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwa mujibu wa sheria.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Uwekezaji,Biashara na Viwanda kwa sasa inafanya marekebisho ya sheria zinazokwamisha utekelezaji wa biashara,Viwanda na uwekezaji nchini , ili kuwaondolea vikwazo wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa uhuru na kuwataka wafanyabishara kushiriki kikao kilichoandaliwa na Wizara ya fedha na Mipango kitakachofanyika januari 11,2023 ili kuwasilisha changamoto wanazokabiliana nazo na kupatiwa ufumbuzi.
Aidha,ametoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini kutunza kumbukumbu za biashara zao na kuitaka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kuwafundisha wafanyabiashara namna bora ya utunzaji wa kumbukumbu za biashara zao ili kutokomeza malalamiko ya kubambikiziwa kodi yanayotolewa na wafanyabiashara.
Lakini pia amesema kuwa, Wizara ya Uwekezaji,Biashara na Viwanda inafanya mawasiliano na Wizara ya fedha na Mipango kufanya marekebisho ya sheria ya kodi ili utekelezaji wa tamko la Rais alilolitoa Mkoani Kagera la kutokukusanya kodi za nyuma ufanyike.
Pia ametoa rai kwa wafanyabiashara nchini kuwa waaminifu katika biashara wanazozifanya ikiwa ni pamoja na wakulima wa parachichi,kwa kutokuuza parachichi ambazo hazijakomaa vizuri ili kutoharibu soko la bidhaa hiyo adhimu duniani kwa sasa ,kwani Serikali imefanya jitihada kubwa ya kutafuta masoko ili kuwainua wakulima na wafanyabishara wa hapa nchini.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa