Na. Lina Sanga
Arusha
Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Ofisi ya Rais,utawala bora na utumishi amezitaka taasisi zote za Umma kuhakikisha sheria,kanuni na viwango vya miongozo ya Serikali mtandao zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanaomba na kupatiwa kibali cha Serikali mtandao kabla ya kutekeleza miradi ya TEHAMA.
Mhe. Jenista alitoa agizo hilo jana kabla ya kufunga kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao,kilichofanyika jijini Arusha katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa- AICC.
Amesema kuwa, taasisi zote za Umma lazima zitumie mifumo shirikishi iliyopo badala ya kila taasisi kuwa na mifumo yake na kuhakikisha mifumo yote inayojengwa na kukaguliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao inakuwa endelevu na kuwataka Makatibu Tawala wa Mikoa kuandaa vikao ngazi ya Mikoa vya kutathmini utendaji kazi unaohusu Serikali Mtandao katika ngazi ya Mikoa hadi Wilaya.
Aidha,amezitaka taasisi, idara na Vitengo kutenga bajeti za mafunzo ya matumizi ya mifumo na kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika na kuwataka Makatibu Tawala wa Mikoa kupima utekelezaji wa matumizi sahihi ya mifumo katika ngazi ya Serikali za mitaa hasa mifumo ya ukusanyaji mapato kwani kuna udanganyifu.
"Wakusanyaji wa mapato wengi hufanya udanganyifu wa matumizi ya mifumo, unapodai risiti wanasema mtandao upo chini kwa kufanya uhalibifu wa makusudi ili wasitoe risiti na kwa sasa dawa ya suala hili imeshapatikana,upigaji sasa basi",alisema Mhe. Jenister.
Aidha,ameitaka Mamlaka ya Serikali mtandao kuendelea kujenga mifumo tumizi na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa ukaribu na zenye ubora.
Pia amezitaka kamati za TEHAMA kukutana na kufanya kazi na kupima matokeo ya usimamizi wa kamati hizo kwa kila taasisi na kuwataka washiriki wote wa kikao hicho kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mifumo kwa watumishi wote na kuhakikisha wanafanyia kazi maazimio yote ya kikao kazi hicho.
Ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kutengeneza mfumo mpya wa mishahara ya watumishi wenye uwezo wa kuhuisha orodha ya mishahara kwa siku moja badala ya siku 14 na kuondoa watumishi wanaostaafu au kufariki ndani ya muda na baada ya kuingizwa taarifa za kifo.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa