Na. Lina Sanga
Bibi Yuditha Mangula (78), mkazi wa Kijiji cha Ibatu Kitongoji cha Isaula,Kata ya Kitandililo katika Halmashauri ya Mji Makambako ambaye ni mnufaika wa TASAF kwa miaka nane sasa,ameishukuru Serikali kwa kumfadhili kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii – TASAF kwa kumpa mradi wa nguruwe na kukuza pato la kaya.
Bi. Yuditha amesema kuwa,mwaka 2017 kupitia TASAF alipata nguruwe tatu dume moja na jike mbili baada ya muda aliuza nguruwe wawili, kila mmoja kwa shilingi 200,000 na kupata jumla ya shilingi 400,000 ambapo alinunua mbuzi mmoja jike kwa shilingi 50,000 na ng’ombe jike mmoja kwa shilingi 350,000 na kwa sasa ng’ombe huyo anatarajia kuzaa.
“Niliamua kubadilisha nguruwe na kuanza kufuga mbuzi kutokana na hali halisi ya eneo letu kwani naona huku mbuzi ni rahisi kumhudumia kuliko nguruwe,ng’ombe nilipomnunua nimemuhamishia Kijiji cha Idete kwa kaka yangu anisaidie kumtunza kutokana na uzee siwezi muhudumia ipasavyo”,alisema Bi. Yuditha.
Ameishukuru Serikali kwa kumuwezesha kupitia ufugaji na fedha anazopewa na TASAF kila baada ya miezi mitatu zinamsaidia katika shughuli za kilimo cha mahindi na maharage ,matumizi ya nyumbani na matibabu.
Ametoa wito kwa wanufaika wote wa TASAF kufanya mabadiliko kupitia miradi wanayopewa na TASAF kwa kuihudumia vizuri ili iweze kuwapa kipato na kubadili hali za maisha katika kaya zao na kuwasaidia watoto ndani ya nyumba.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa