Na. Lina Sanga
Kauli hiyo imetolewa na Bi. Roida Mposola mwenye umri wa miaka 60 mkazi wa kijiji cha Mawande,Kata ya Utengule katika Halmashauri ya Mji Makambako ambaye ni mnufaika anayefadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) tangu 2015.
Bi. Roida ambaye ni mjane amesema kuwa,mwaka 2017 kupitia TASAF alipewa nguruwe wawili, jike na dume ambao aliweza kuwafuga na kuzalisha kwa awamu tatu na kufanikiwa kupata fedha ambazo zilimuwezesha kujenga nyumba ya tofali baada ya nyumba yake ya awali iliyojengwa kwa udongo kubomoka kutokana na mvua.
Nguruwe wanaofugwa na Bi. Roida Mposola.
“Walipokuja kuandikisha kunusuru kaya masikini mvua ilikuwa imenyesha na ndani kumelowa kwa sababu ilikuwa inavuja hata sehemu ya kuweka viti wakae watu wawili haikuwezekana,baada ya kupata msaada wa TASAF na kupewa fedha za kujikimu kila baada ya miezi miwili niliweza kujikusanya kidogo kidogo na kuwekeza kwenye kikundi cha maendeleo cha TASAF cha kuweka na kukopa cha hapa kijijini na kufanikiwa kuanza ujenzi wa nyumba ya tofali na kuezeka bati”,alisema Bi. Roida.
Nyumba ya Bi. Roida aliyoijenga baada ya kuwezeshwa na TASAF.
Nyumba ya awali ya Bi. Roida ambayo ilibomoka kabla ya kufikiwa na TASAF 2015.
Aidha amebainisha kwamba,Mwaka 2017 TASAF ilimpa mradi wa ufugaji wa nguruwe wawili jike na dume, ambapo alifanikiwa kupata vitoto 19 kwa awamu tofauti,awamu ya kwanza nguruwe huyo alizaa vitoto saba ambavyo aliuza kila kimoja kwa shilingi 50,000,awamu ya pili alizaa vitoto 6,awamu ya tatu vitoto sita ambavyo aliuza kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa nyumba ambapo mwaka 2017 nguruwe mkubwa aliuzwa shilingi 250,000 na vitoto shilingi 50,000.
“Baada ya kukabidhiwa hao nguruwe hata pombe niliacha nilikuwa nashinda vilabuni kulewa lakini nilijiuliza Serikali na TASAF wamenionaje mimi na sio wenzangu wenye hali kama yangu?, kutoka moyoni niliamua kuacha pombe na kuanza kuwatunza nguruwe niliopewa na nilifanikiwa kupata vitoto 7 kwa uzao wa kwanza nikauza vyote na kuanza kuwekeza kwa ajili ya tofali na bati kwa sasa namiliki nyumba nzuri na mpango wangu kwa sasa ni kujenga choo cha kisasa na jiko”,alisema Bi. Roida.
Ametoa shukurani kwa Serikali kupitia TASAF kwa kumuwezesha kumiliki nyumba ya bati na kupitia ufugaji wa nguruwe na utengenezaji wa vyungu anapata fedha za kumsomesha mjukuu wake na kuendesha maisha.
Baadhi ya vyungu vinavyotengenezwa na Bi. Roida ambavyo huuza kuanzia 500 na kupata fedha za kujikimu kimaisha.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa