Na. Lina Sanga
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Augustino Ngunde amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka kwa kuibua mradi wa parachichi kwa ajili ya wanufaika wa TASAF,kwani kupitia mradi huo changamoto za umasikini zitapungua.
Ngunde, ametoa kauli hiyo leo katika ziara ya Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. Deogratius Ndejembi katika Halmashauri ya Mji Makambako ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Amesema kuwa mradi wa parachichi kwa wanufaika wa TASAF ni mradi mpya na Serikali imekuwa isisitiza kutambuliwa kwa miradi hiyo kama miradi mingine ya Serikali,hivyo Mkoa wa Njombe umeongeza nguvu katika kupiga vita Umasikini na Mikoa mingine ione namna inavyoweza kufanya ili kutokomeza umasikini.
Ameongeza kuwa endapo wanufaika wa TASAF watazingatia mradi huo changamoto za umasikini zitapungua kwani utasaidia kwa kipindi kirefu,hivyo ni wajibu wa kila mtu kuunga mkono juhudi za viongozi wa Mkoa katika kufanikisha mradi huo.
Aidha,amewapongeza wananchi wa Mtaa wa Magongo kwa ushiriki wao katika utekelezaji wa ujenzi wa madarasa katika shule ya Msingi shikizi ya Magongo na kukamilisha mradi kwa haraka.
Zaidi ya Mil. 134 za TASAF kwa mwaka wa fedha 2021/2022,zilitumika kujenga vyumba 5 vya madarasa na ofisi moja,matundu 12 ya vyoo vya wanafunzi na walimu katika Shule ya msingi shikizi ya Magongo, ambayo imepunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya Msingi Juhudi iliyokuwa ina wanafunzi zaidi ya 1,000 na ina jumla ya wanafunzi 124 wa darasa la awali hadi la sita kwa sasa.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa