Na. Lina Sanga
Iringa
Watanzania wametakiwa kuungana na kukumbushana kuhusu uchomaji moto kiholela hasa nyakati za uandaaji mashamba,kwa kutafuta njia mbadala za kuandaa mashamba badala ya moto ili kutunza na kuhifadhi vivutio vya utalii pamoja na misitu.
Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Dkt.Pindi Chana(Mb) katika ufunguzi wa maonyesho ya utalii karibu kusini 2022, yanayofanyika Mkoani Iringa.
Mhe. Chana amesema kuwa Moto ni changamoto kubwa sana katika uhifadhi wa misitu na vivutio vya utalii kwani unasababisha uharibifu mkubwa kwa muda mfupi,na kuwataka watanzania wote kushiriki kudhibiti hasara za moto kwa kuacha kuchoma mashamba ovyo.
Amesema kuwa Serikali inatumia gharama kuvitangaza vivutio vya utalii ili kuzalisha ajira kwa watanzania na kuongeza pato la taifa,hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuwa mlinzi wa mwenzake juu ya matumizi holela ya moto mashambani kwa maslahi ya umma.
Pia ametoa wito kwa wananchi kuhifadhi mazingira na kutunza vyanzo vya maji ili kukabiliana na ukosefu wa maji kwa kutopitisha mifugo kwenye vyanzo hivyo na kufanya shughuli za kibinadamu ikiwamo kilimo na kuilinda misitu kuepusha jangwa kwa kudhibiti moto.
Aidha Mhe. Chana amesema zaidi ya bil. 12 zitatumika kujenga kituo cha kutolea taarifa za utalii mikoa ya kusini katika eneo la maonyesho la utalii karibu kusini lililopo Kihese Kilolo,Mkoani Iringa kwani maonyesho hayo ni utekelezaji wa mikakati ya Serikali kufungua utalii Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.
Ametoa wito kwa watanzania na wawekezaji wa nchi zingine kuwekeza katika mikoa ya Kusini kwa ujenzi wa hoteli zenye hadhi ya kimataifa,ujenzi wa kambi kwa kutumia hema na huduma nyingine muhimu kama chakula cha asili ili kuwavutia watalii na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa