Na. Lina Sanga
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Uratibu na Bunge,Mhe.Balozi Dkt.Pindi Chana(Mb) amepongeza ujenzi wa jengo la kutolea huduma ya vipimo na tiba kwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (CTC),katika kituo cha afya Cha Makambako.
Mhe. Chana amesema kuwa kwa sasa jukumu lililobaki ni kuwajulisha wananchi juu ya uwepo wa jengo hilo,katika kituo cha afya makambako ili waweze kupata huduma hiyo na kuwa zinatolewa muda wote pasipo malipo.
“Kuwa na kituo ni kitu kimoja na kukitumia ipasavo ni kitu kingine, wanahabari mnapaswa kuendelea kuwahabarisha wananchi kwamba kituo hiki kipo,pia kuanzia tarehe nane, wahudumu wa afya nyinyi ndiyo mtakaoendelea kuhubiri juu ya uwepo wa kituo hiki,na huduma zake kwa mujibu wa maelekezo na sera yetu ya afya kwamba huduma hizi zinatolewa pasipo malipo na zinatolewa muda wote kwani magari ya masafa marefu yanapita muda wote”,alisema Dkt. Chana.
Pia ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa sababu kupitia yeye, dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania inaonekana ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya na maeneo mengine katika Nchi.
Aidha,Dkt. Pindi amempongeza meneja wa TANROADS mkoa wa Njombe kwa jitihada mbalimbali anazofanya katika utekelezaji wa majukumu yake,ikiwa ni pamoja na kusimamia ujenzi wa madaraja yaliyobomoka wilaya ya Ludewa kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha,kwa kuhakikisha madaraja yanakamilika ili matumizi ya barabara yaendelee.
Mwisho ametoa wito kwa wananchi wote kuzitumia huduma zinazotolewa na kituo hicho cha CTC,kwani kutambua afya ni vizuri na kuchukua tahadhari.
Mhe. Pindi Chana (Mb) amefanya ukaguzi wa jengo la CTC lililopo katika kituo cha afya Makambako leo,ambalo limejengwa na TANROADS Mkoa wa Njombe ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ujenzi wa Barabara kuu inayounganisha Mkoa wa Iringa,Njombe na Mbeya na Nchi jirani kama Zambia na Malawi.
Ujenzi wa jengo hilo umekamilika kwa asilimia mia moja na limegharimu jumla ya shilingi Mil.252.8,na makabidhiano ya jengo hilo kati ya TANROADS na Uongozi wa Halmashauri ya Mji Makambako unatarajiwa kufanyika machi 8,2022.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa