Na. Lina Sanga
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Kenneth Haule amewataka wananchi wote ambao maeneo yao hayajapimwa, kuunga mkono jitihada za Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupunguza gharama za urasimishaji ili wananchi wote hadi wa hali ya chini wapimiwe maeneo yao.
Haule ametoa wito huo leo katika Mtaa wa Mlando mara baada ya wananchi kuibua hoja ya kusuasua kwa baadhi ya wananchi kulipa gharama za urasimishaji kwa madai ya kusubiri zoezi hilo lianze kutekelezwa ndipo walipe,kwa kuhofiwa kudhulumiwa fedha na Serikali.
Amesema kuwa ,kuchelewa kwa utekelezaji wa zoezi hilo ni kutokana na masuala mbalimbali ya kiutendaji na maagizo ya wizara ya ardhi ya namna ya kutekeleza zoezi hilo, ikiwa ni pamoja suala la gharama ili kila mwananchi apate fursa ya kupimiwa kipande cha ardhi anayomiliki na kupata hati ambapo awali zoezi hilo lilitekelezwa kwa gharama tofauti tofauti kuanzia 300,000 hadi 250,000 na kwa sasa Serikali imepunguza gharama hadi 130,000 ili wananchi wa hali ya chini waweze kumudu na kurasimishiwa ardhi zao.
"Ndugu zangu Serikali inapoleta jambo jitahidi kulifanya kwa wakati ili kupata huduma kwa gharama ndogo,mkumbuke gharama ya kuunganishiwa umeme ilishushwa hadi sh. 27,000 kuna watu waliounganisha na kuna wale waliojivutavuta hadi leo hawajaingiza umeme kutokana na gharama kuongezwa,ndivyo itavyokuwa kwenye zoezi hili na mimi kama mkurugenzi pamoja na watumishi wangu tumekuja kunawa mikono maana mkaidi hafaidi mpaka siku ya idi", alisema Haule.
Ametoa wito kwa wananchi ambao wamepanga kusubiri kazi ya urasimishaji ianze ndipo walipie,kuanza kulipia gharama hizo ndani ya muda uliopangwa kwani kazi haiwezi kuanza bila ya fedha kuingizwa kwenye akaunti na kila mwananchi ana wajibu wa kuchangia fedha hizo kwani urasimishaji ni takwa la kisheria.
Naye, Obert Sigala Mkazi wa Mtaa wa Mlando, ametoa rai kwa Mkurugenzi kuendelea na zoezi la urasimishaji kwa watakaolipa ndani ya muda husika, kwani baadhi ya watu wana tabia ya ukaidi hadi itumike nguvu.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa