Na. Lina Sanga
Uongozi ngazi ya Kata,Mitaa na Vijiji umetakiwa kuhakikisha maeneo yote ya huduma za jamii yanapimwa na kuwa na hati miliki ili kuepuka migogoro ya ardhi.
Rai hiyo imetolewa leo na wajumbe wa Kamati ya fedha na uongozi katika ziara ya kamati hiyo ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha kuishia robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mhe. Hanana Mfikwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya fedha na uongozi amesema kuwa, uongozi wa Kata, Mitaa na Vijiji wanawajibu wa kuanzisha michakato ya kupata hati miliki ya maeneo ya huduma za kijamii kama vile shule,zahanati na vituo vya Afya ili kuepuka migogoro ya ardhi kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi kupitia wataalamu wa idara ya Ardhi.
Aidha, ametoa rai kwa walimu kusimamia ulinzi wa miundombinu inayojengwa kwa kuhakikisha marekebisho yanafanyika pindi wanafunzi wanavyovunja vioo au madawati kwa kushirikiana na wazazi ili miundombinu hiyo itumike muda mrefu.
Pia, amewapongeza wananchi kwa kujitoa kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye maeneo yao,ikiwa ni pamoja na usimamizi na umiliki wa miradi kwa kufuatilia kila hatua ya utekelezaji.
Kamati ya fedha na uongozi leo imetembelea miradi mitano ambayo ni ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mawande Kata ya utengule,Ujenzi wa nyumba pacha ya walimu katika shule ya msingi Deo Sanga katika Kata ya Mahongole,ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya sekondari Kitandililo,Kata ya Kitandililo na ujenzi wa jengo la utawala shule ya sekondari Kitisi katika Kata ya Kitisi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa