Na. Lina Sanga
Njombe
Utaratibu wa mama mjamzito kufika kliniki pamoja na mwenza wake ili aweze kupata huduma,ni moja ya chanzo cha baadhi ya watoto kukosa lishe tangu wakiwa tumboni.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa katika kikao cha utiaji saini mikataba ya lishe kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe, ambapo imedaiwa kuwa Mkoa wa Njombe una asilimia 53.6 ya watoto wenye udumavu.
Mhe. Kissa amesema kuwa, utaratibu uliowekwa katika vituo vya kutolea afya kumtaka mama mjamzito kufika na mwenza wake kliniki,ndipo ahudumiwe ni kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanawake hasa kwa waliobakwa na wenye wenza ambao hawaeleweki au waliozaa na waume za watu,hali inayopelekea kina mama wengi kutofika kliniki hadi wanapojifungua na kupata huduma za msingi kwa manufaa yao na watoto walio tumboni.
Mhe. Kissa amesema ipo haja ya utaratibu huo kutazamwa kwa namna nyingine ili wanawake waweze kufika kliniki,na kupewa elimu ya lishe na kupata huduma nyingine muhimu kwa mama mjamzito ikiwa ni pamoja na kupima afya na Wilaya ya Njombe utaratibu huo umeanza kutizamwa upya ili kupunguza kikwazo cha mama mjamzito kupata huduma za kliniki.
Aidha,ameongeza kuwa licha ya sababu mbalimbali zilizobainishwa kusababisha udumavu katika Mkoa wa Njombe,Mhe. Kissa amesema kuwa ipo haja ya tafiti nyingine kufanyika hasa kuhusu hali ya baridi katika Mkoa wa Njombe,kwani huenda nayo ni sababu ya udumavu wa watoto kwani kama mifugo inachelewa kukua kutokana na baridi huenda hata binadamu wanaathiriwa na baridi katika ukuaji.
Ametoa wito kwa maafisa lishe kuwatumia watendaji wa mitaa na vijiji ili kupata takwimu sahihi za lishe,badala ya kuwauliza watu moja kwa moja kwani baadhi ya watu wanatoa takwimu za uongo na kuwataka wananchi kujenga mazoea ya unywaji maziwa kwa ajili ya afya zao.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa