Na. Lina Sanga
Vijana wametakiwa kushiriki shughuli za maendeleo katika Kata,Mitaa na Vijiji wanavyoishi,ili kuboresha huduma muhimu za kijamii kama ujenzi wa shule,zahanati na vituo vya afya kwa maslahi ya familia zao.
Wito huo umetolewa na Mbunge wa jimbo la Makambako,Mhe. Deo Kasenyenda Sanga baada ya kupokea malalamiko ya wazee wa Mtaa wa Igangidung’u katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo katika Ofisi za Mtaa huo.
Mhe. Sanga amesema kuwa vijana wote kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea,hawana budi kushiriki shughuli zote za maendeleo katika mtaa wanaoishi hata kama hawana watoto kwa sasa.
Amesema kuwa mtaa huo una changamoto ya ukosefu wa zahanati na shule ya msingi,ili Serikali ilete fedha wananchi wanatakiwa kuibua miradi ya ujenzi ndipo Serikali italeta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo ambayo wananchi wameanza kuyajenga kwa nguvu zao.
“Kwani mimi najenga madarasa yote na shule nachangia nina watoto wanaosoma?,kwenye maendeleo hakuna cha kusema wewe una mtoto au huna mtoto maadamu unakaa kwenye eneo husika unatakiwa kushiriki kwenye shughuli za maendeleo,waliodai uhuru wa nchi hii walikuwa wachache lakini tunaofaidi ni wengi,hivyo maendeleo tutayoyafanya hapa wataofaidi ni vizazi vyote vya Igangidung’u vilivyopo na vijavyo hivyo suala la maendeleo ni lazima kila mtu kushiriki”, alisema Mhe. Sanga.
Ametoa wito kwa wakazi wote wa Mtaa huo kushikamana kwa pamoja na kumsikiliza Mwenyekiti wa Mtaa,na mamlaka yake ili waweze kufanya maendeleo ya shule katika mtaa huo.
Aidha,ameuagiza Uongozi wa mtaa huo kufanya mazungumzo na mmiliki wa eneo ambalo wanahitaji kujenga shule,na endapo kuna changamoto yoyote kuhusu gharama ya fidia watoe taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako ili taratibu za Seriikali zifanyike na hatimaye ujenzi uanze.
Pia,amemuagiza Mtendaji wa Kata ya Kivavi kukaa na Kamati ya Maendeleo ya Kata(KAMAKA) ili kuanza mchakato wa kupata eneo, kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ili kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kufuata huduma za afya mbali na mtaa wao.
Ziara ya Mbunge wa jimbo la Makambako,Mhe. Deo Kasenyenda Sanga leo imefanyika katika mtaa wa Malombwe,Kata ya Lyamkena na Mtaa wa Igangidung'u na Kibedange katika Kata ya Kivavi na kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zao,kutoa jumbe mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/2023,Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23,mwaka huu, mbolea ya ruzuku na kuhamasisha chanjo ya uviko 19 na jumla ya watu 66 wamepata chanjo hiyo.
#jiandaekuhesabiwa2022
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa