Na. Lina Sanga
Viongozi wa dini wametakiwa kuwahamasisha waumini wao kupata huduma za afya ya uzazi,kwani hata wataalamu wa afya wamepewa vipawa hivyo na Mungu kwa ajili ya kuwasaidia wanadamu.
Rai hiyo imetolewa na Joynetta Saria,Afisa jamii hospitali ya Marie Stopes katika kikao cha MTAKUWA kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Makambako,kwa ajili ya kupokea mrejesho wa shughuli za uelimishaji masuala ya ukatili na afya ya uzazi,zilizofanyika agosti 16,mwaka huu kupitia ushirikiano wa shirika la JEUMA na hospitali ya Marie Stopes Makambako.
Saria amesema kuwa baadhi ya viongozi wa dini huwashawishi waumini wao kutohudhuria kliniki za masuala ya afya ya uzazi na kujiunga na huduma hizo,kwa madai ya kuwaombea hali inayosababisha ongezeko la vifo kutokana na uzazi.
Naye,Afande Happy Edward kutoka ofisi ya dawati linaloshughulikia masuala ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kutoka kituo cha polisi Makambako ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwaelewesha vizuri waumini wao juu ya maandiko mbalimbali kutoka kwenye vitabu vitakatifu,ili waweze kutafsiri maandiko hayo ipasavyo na kuepuka kuyatumia kutekeleza ukatili kwa wengine.
Afande Happy amesema kuwa,baadhi ya wanaume hutumia neon la mwanaume ni kichwa cha familia lililopo katika biblia,kuwanyanyasa na kuwakatili wake zao hali inayosababisha kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa wanawake na watoto.
Naye,Afande Manyumba Edward ametoa rai kwa viongozi wa dini na jamii kurejea nyakati za zamani kwa kufuata misingi ya dini ipasavyo,ili kuwawezesha watoto kukua katika maadili ya dini zao ili kutokomeza vitendo vya kikatili katika familia na jamii kwa ujumla.
Afande Manyumba amesema kuwa,shule za jumapili katika ibada (Sunday school) na madrasa kwa upande wa dini ya kiislamu husaidia kumkuza mtoto katika maadili ya dini,kumfundisha namna ya kuishi kwa kujijali mwenyewe na kuwajali wengine pamoja na kuwa na upendo na wengine,hali inayomsaidia mtoto kuepuka kujiingiza katika vitendo visivyofaa katika jamii.
MTAKUWA ni ufupisho wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto nchini Tanzania.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa