Na. Lina Sanga
Wazazi wenye watoto wenye umri wa kuanza darasa la awali wametakiwa kuwaandikisha watoto hao kwenye shule rasmi ,badala ya kuwaandikisha kwenye vituo vya kulelea watoto na shule za chekechea ambazo ni rasmi kwa ajili ya watoto walio chini ya umri wa miaka minne.
Wito huo umetolewa leo na Mwl. Erasto Nyagawa, Afisa elimu vifaa na takwimu wa Halmashauri ya Mji Makambako wakati akitoa takwimu za uandikishaji wa wanafunzi wanaotarajia kuanza masomo ya darasa la awali na la kwanza mwaka huu, ikiwa zimebaki siku nne za kuanza rasmi muhula wa masomo kwa mwaka 2024.
Mwl. Nyagawa amesema kuwa,zoezi la uandikishaji katika shule za msingi zilizopo Halmashauri ya Mji Makambako linaendelea na hadi kufikia leo januari mosi, jumla ya wanafunzi wa 2,253 wa darasa la awali wameandikishwa ,wavulana 1,123 na wasichana ni 1,130 ikiwa ni sawa na asilimia 55 na wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa ni 3,793 ambapo wavulana ni 1.878 na wasichana ni 1,915 sawa na asilimia 96.
Amesema kuwa,uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali asilimia yake ni ndogo kutokana na changamoto ya baadhi ya wamiliki wa vituo vya kulelea watoto na shule za chekechea kupokea wanafunzi wenye umri wa miaka 4 hadi 5 ambao wanatakiwa kuanza darasa la awali na baadhi ya wazazi kuwapeleka watoto hao kwenye vituo hivyo ili kupata urahisi wa malezi ya watoto hasa kwa maeneo ya Mjini.
Ametoa rai kwa wazazi ambao bado hawajawaandikisha watoto kufika katika shule zilizo karibu na maeneo yao ,kwani elimu ni haki ya kila mtoto aliyefikia umri wa kuanza masomo na zoezi la uandikishaji linaendelea hadi machi 31,2024.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa