Na. Lina Sanga
Njombe
Wabunge wa Mkoa wa Njombe wametoa rai kwa Wakala wa barabara Vijijini (TARURA), kushughulikia maeneo korofi katika barabara zinazotarajiwa kufanyiwa matengenezo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ili ziweze kupitika kwa mwaka mzima.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Lupembe,Mhe. Edwin Swalle kwa niaba ya wabunge wote wa majimbo ya Mkoa wa Njombe,katika kikao cha utiaji saini mikataba ya matengenezo na ukarabati wa barabara na ujenzi wa madaraja,kwa mwaka wa fedha 2022/2023,kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Mhe. Swalle amesema kuwa,wabunge kwa pamoja wametoa rai hiyo kwani mkoa wa Njombe ni Mkoa wa Mvua,TARURA wanaweza jenga barabara yenye urefu wa kilomita 10 au 20,lakini eneo korofi linalofanya barabara hiyo isipitike kwa mwaka mzima halifanyiwi matengenezo kwa kuwa halipo katika bajeti husika.
Amesema kuwa,dhamira ya Mhe.Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuongeza bajeti ya barabara ni kujenga barabara,ili ziweze kupitika kwa mwaka mzima na wananchi waweze kusafirisha mazao kwenda sokoni,kusafirisha wagonjwa na huduma kwa wananchi.
Naye,Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Njombe,ametoa rai kwa wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya ujenzi,kulipa kodi kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla,kwani fedha zinazokusanywa na mamlaka hiyo ndiyo zinatumika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya Mkoa na taifa kwa ujumla.
Kenneth Haule,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako,kwa niaba ya Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji na Wilaya za Mkoa wa Njombe ametoa rai kwa Wakala wa barabara Vijijini (TARURA),kuweka utaratibu mzuri katika mfumo wa malipo ili wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara katika Halmashauri waweze kulipa kodi ya huduma ili kuongeza mapato ya Halmashauri.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa