Na. Lina Sanga
Njombe
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka kwa Wakala wa Misitu nchini(TFS), kuboresha na kutumia Mifumo ya TEHAMA,katika utoaji wa vibali vya kusafirisha mazao ya misitu ili kupunguza urasimu na kuwawezesha wafanyabiashara kupata vibali popote na wakati wowote wanapohitaji.
Mhe. Mtaka alitoa rai hiyo jana katika Mkutano wa saba wa baraza la biashara Mkoa wa Njombe,uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe na kuhudhuriwa na Waziri wa Uwekezaji,Biashara na Viwanda,Mhe. Ashatu Kijaji baada ya kusikiliza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wafanyabiashara katika Mkoa huo.
Katika mkutano huo wafanyabiashara walipata fursa ya kutoa changamoto zao na ushauri kwa Serikali,ili kupata ufumbuzi wa baadhi ya vikwazo visivyo na ulazima katika sekta ya biashara ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kupata kibali cha kusafirisha mbao na kuhuisha kibali baada ya kupata changamoto ya usafiri.
Mhe.Mtaka amesema kuwa, utaratibu wa kupata kibali katika ofisi za Wakala wa Misitu ni utaratibu uliopitwa na wakati, hivyo ni vema Wakala wa Misitu kuboresha mfumo wa utoaji wa vibali kutoka mfumo wa analogia hadi mfumo wa kidigitali ili mfanyabiashara aweze kulipia kibali wakati wowote na mahali popote na aruhusiwe kuuza soko lolote katika Mji unaosomeka kwenye kibali cha usafirishaji.
Aidha,Mhe. Mtaka amewataka wafanyabiashara katika sekta ya usafirishaji wa daladala na bajaji, kuachana na migogoro baina yao ya kugombea wateja kwani kwa sasa hali ya maisha imebadilika na mteja ana uhuru wa kuchagua aina ya usafiri anaoutaka na sio kulazimishwa.
Naye Mbunge wa jimbo la Njombe Mjini, Mhe. Deo Mwanyika ametoa rai kwa Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda kuwasaidia wakulima wa zao la chai kupata soko la uhakika, ili wakulima waweze kunufaika kwa kuuza chai kwa bei nzuri.
Pia ametoa wito kwa Serikali kuwekeza kwenye zao la parachichi mapema ili wakulima wa zao hilo baada ya miaka mitano wasipate hasara, kwani idadi ya wananchi waliohamasika kuwekeza kwenye kilimo cha parachichi inaongezeka siku hadi siku.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa