Na. Lina Sanga
Wakazi wa Mkoa wa Njombe wametakiwa kuchangamkia fursa za mfumo wa stakabadhi za ghala, ili waweze kufanikiwa kupitia mazao na bidhaa wanazozalisha na kupata tija zaidi.
Wito huo umetolewa leo na Kaimu Meneja uratibu huduma wa Bodi ya usimamizi wa stakabadhi za Ghala,Erick Temu katika kikao na Madiwani na Wataalamu wa Halmashauri ya Mji Makambako, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Temu amesema kuwa, mfumo wa stakabadhi za ghala ni mfumo wa masoko unaomuwezesha muweka mali kuweka mali kwenye ghala lenye leseni na kumuwezesha mzalishaji au mkulima kupata soko la uhakika kupitia taarifa za mali husika zilizoandikwa na ubora wa bidhaa ambazo zinatangazwa kwa wadau wengi waliopo kwenye mfumo huo.
Amesema kuwa, mfumo huo pia unampa nafasi mzalishaji mali hususani mzalishaji mali na mkulima mdogo,ambaye hana uwezo wa kufikisha mali zake sokoni,kufikisha mali zake sokoni kwa kutumia utaratibu wa ghala kupitia chama cha msingi,ambapo wakulima na wazalishaji wengine wanakusanya mali zao katika ghala la chama cha msingi na kusafirisha kwenda kwenye ghala kuu na kuingizwa katika kanzidata ya mfumo,na kila mdau ambaye yupo kwenye mfumo anaziona na bei itatangazwa na mnunuzi wa bei ya juu atapewa mzigo huo.
Ametaja manufaa ya mfumo huo kuwa ni pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana kama kubeba mizigo,biashara ya chakula na nyumba za kulala wageni,kwani ghala linakutanisha watu wengi kutoka maeneo mbalimbali hivyo uchumi wa wakazi wa eneo husika unaongezeka na mkulima anapata manufaa kwa kupata soko la uhakika na kuuza bidhaa kwa bei nzuri.
Aidha, ameongeza kuwa,mfumo wa stakabadhi za ghala Unaleta utambuzi wa bidhaa ambao unawasaidia wazalishaji na wakulima, kutambulika sehemu wanayopatikana kwa urahisi na kuongeza wigo wa soko la bidhaa zinazozalishwa katika eneo husika.
Pia,amebainisha kuwa kukosekana kwa ghala kunasababisha changamoto ya udhibiti wa bei ya uhakika ya bidhaa mbalimbali,hivyo mfumo wa stakabadhi za ghala utamsaidia mkulima na mzalishaji mali mdogo kupata tija katika kilimo na bidhaa anazozalisha.
Ametoa rai kwa wamiliki wa maghala ambao wanahitaji kuingia kwenye mfumo huo, kuhakikisha sehemu ambayo mazao yanahifadhiwa, hayataharibiwa au kunyeshewa na mvua na yataweza kuhifadhiwa kwa kiwango ambacho kinatosha uhifadhi wa eneo husika.
Bodi ya usimamizi wa stakabadhi za Ghala ni taasisi ya Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara,yenye mamlaka ya kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za Ghala,ambao unawezesha mazao au bidhaa kuhifadhiwa ndani ya ghala zenye leseni.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa