Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Makambako,Kenneth Haule alipokuwa akijibu hoja ya Mhe. Imani Fute diwani wa kata ya Kitandililo katika mkutano wa Baraza la Madiwani,lililofanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri kuhusu utoaji elimu kwa wakulima juu ya uchaguzi wa mbolea bora kutokana na kupanda bei ya Mbolea nchini kwani matangazo ya biashara ya mbolea kwa sasa ni mengi hali inayoweza kuwachanganya wakulima.
Akijibu hoja ya kupanda bei kwa mbolea,Bw,Haule amesema kuwa mbolea zinazotumika nchini,zinazalishwa nchi za nje na waziri mwenye dhamana ameshatoa tamko juu ya suala la bei za mbolea kupanda,lakini licha ya kupanda bei kwa mbolea nchini,wakulima wengi wa Makambako bado wanalima kwa mazoea kwani mbolea walizozizoea kutumia ni DAP,UREA na CAN,hata wanapoelekezwa aina ya mbolea ambayo ni nzuri na inauzwa bei ya chini kuliko mbolea hizo hawapo tayari kuzitumia.
“Katika mji wetu wa Makambako,wakulima wengi wamezoea aina tatu za mbolea DAP,UREA na CAN, na mbolea hizo kwa sasa bei zipo juu kwa mfano DAP inauzwa Tshs. 110,000 mfuko mmoja,lakini mbolea aina ya NPS inauzwa Tshs. 95,000 mfuko mmoja,lakini mkulima haoni unafuu wowote kati ya bei ya kununua DAP na NPS kwa sababu amezoea kutumia DAP,licha ya hayo yote timu ya wataalamu wa kilimo itaendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wakulima juu ya matumizi ya mbolea”,alisema Bw. Haule.
Aidha Bw. Haule amesema kuwa kinacho wakwamisha wakulima katika matumizi bora ya mbolea ni pamoja na kulima maeneo makubwa kuzidi uwezo wao wa kuyahudumia, kwa matarajio ya kupata mavuno mengi pasipo kutambua kuwa ukubwa wa eneo sio wingi wa mavuno,bali huduma ya mazao yaliyopo shambani.
Ametoa wito kwa wakulima kulima maeneo madogo kulingana na uwezo wa kupata pembejeo za kilimo,kama mbolea na mbegu bora ili kupata mazao mengi na yenye ubora,lakini pia matumizi ya mbolea ya samadi ili kuepukana na gharama za ununuzi wa mbolea za kiwandani,kwani samadi inapatikana kiurahisi na kwa gharama nafuu kikubwa ni kuzingatia ushauri wa wataalamu juu ya matumizi ya mbolea hiyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako,Mhe. Salum Mlumbe amewataka watumishi wa Umma kufanya kazi kwa weledi na kuacha utoro na utovu wa nidhamu,baada ya kutangaza kumfukuza kazi mtumishi mmoja wa idara ya Afya,Frank Selestine ambaye alikua afisa muuguzi na kumpunguzia mshahara Boniface Kyando ambaye ni Afisa mtendaji kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Pia Mhe. Mlumbe amewasisitiza watendaji wa kata,mitaa na vijiji kukusanya mapato ya serikali kama inavyotakiwa ili kufikia lengo la ukusanyaji mapato, kwani kwa sasa makusanyo yamefikia asilimia 98.34 lengo ni kufikia asilimia 100 ya makusanyo ya mapato.
MWISHO.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa