Na. Tanessa Lyimo
Walimu wakuu wa shule za awali na msingi 17 katika Halmashauri ya Mji Makambako, wanatarajia kupewa semina ya mafunzo kwa ajili ya kujengewa uwezo wa kufundisha kwa vitendo mtaala mpya wa elimu ya awali na msingi ambao nao watawafundisha walimu wengine katika shule 57 za awali na msingi ndani ya Halmashauri ya Mji Makambako.
Hayo yameelezwa na mwezeshaji kitaifa kutoka Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI),Mwl. Jerome Mwakifuna wakati wa semina ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufundisha kwa vitendo mtaala mpya wa elimu ya awali na msingi timu ya uwezeshaji ngazi ya Halmashauri, iliyofanyika leo katika ukumbi wa shule ya Msingi Sigrid.
Mwl. Mwakifuna amesema kuwa, mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo walimu ili waweze kufundisha kutoka kwenye mfumo wa nadharia na kuweza kufundisha kwa vitendo ili waendane na kasi na mahitaji ya dunia ya sasa yenye ushindani.
Kwa upande wake afisa elimu taaluma divisheni ya elimu ya awali na Msingi katika Halmashauri ya Mji Makambako, Mwl. Shaban Ambindwile amesema kuwa, mafunzo hayo yatawasaidia walimu pamoja na wanafunzi wanaokwenda kutumia mfumo mpya wa Mtaala kuanzia elimu ya awali Mpaka darasa la sita na Halmashauri ya Mji Makambako imejipanga vyema kuhakikisha mafunzo hayo yanawafikia walimu wote baada ya semina hiyo kukamilika.
Naye, Mwl. Furaha Mgeni, kutoka shule ya msingi Lungwa ambaye ni mmoja kati ya timu ya uwezeshaji ngazi ya Halmashauri amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao, katika kuwajengea uwezo wa kuandaa Zana mbalimbali za kufundishia hasa kwa ngazi ya awali, na kuwataka walimu wote kuyapokea mafunzo hayo ili yawasaidie katika ufundishaji.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa