Na. Lina Sanga
Zaidi ya wananchi 180 wa kijiji cha Kifumbe na Usetule,Kata ya Mahongole katika Halmashauri ya Mji Makambako,wamepata chanjo ya Uviko 19 leo,katika Mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa katika ziara ya Kijiji kwa kijiji, Mtaa kwa Mtaa iliyofanyika leo katika Vijiji hivyo.
Mhe. Kasongwa amesema kuwa inasikitisha mpaka sasa kuna baadhi ya wananchi wanakaidi kupata chanjo ya Uviko 19,kwa madai kuwa wazungu wanataka kuwaua na kuwa chanjo hiyo inasababisha upungufu wa nguvu za kiume.
Amesema kuwa asilimia kubwa ya vitu vinavyotumika Nchini vinatoka kwa wazungu,lakini hakuna mtu aliyeacha kutumia vitu hivyo kwa madai ya kupata madhara yoyote au kifo,lakini chanjo ya Uviko 19 pekee.
“Kila mtu hapa amepata chanjo nyingi tangu amezaliwa,kondomu za kiume zikiwekwa ofisi ya kijiji saa 12 jioni,kesho asubuhi zinakuwa zimeisha je,hizo hazitengenezwi na wazungu? kwanini mzungu akuue kwa sindano na sio kondomu? mbolea tunazotumia zinatoka kwa wazungu kwanini wasituue kupitia mbolea?dawa za kufubaza makali ya UKIMWI (ARV) zinatengenezwa na wazungu na wananchi wengi wanazitumia,kwanini hao wazungu wasiwaue kupitia dawa hizo?Wananchi wenzangu acheni visingizio kila mmoja apate chanjo kwa faida yake na familia yake”,alisema Mhe. Kasongwa.
Ametoa wito kwa wananchi wote kuchanja ili kuwa salama kwani Ugonjwa wa korona upo na watu wengi wanafariki kutokana na ugonjwa huo,hakuna mwanaume aliyechanja ameripoti kupungukiwa na nguvu za kiume wala kupata madhara yoyote.
Mhe. Kasongwa amesema kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawezi kuruhusu sumu itumike na watanzania,kwani mtaji wa kila mwanasiasa ni watu na Rais wetu amejiridhisha kuwa chanjo zote zinazoingizwa Nchini ni salama kwa afya za watu,ndiyo maana naye alichanja kudhihirisha kuwa hakuna madhara yoyote katika chanjo ya Uviko 19.
Kenneth Haule,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako pia amewataka wananchi wote kupata chanjo ya Uviko 19,kwani haina madhara yoyote na kila mwananchi anawajibu wa kupata chanjo hiyo kwa usalama wake na watu wengine,Serikali inawajali wananchi wote na ndiyo maana imeleta chanjohiyo bure ili kila mwananchi apate,hivyo kila mwananchi ambaye bado hajachanaja ahakikishe anapata chanjo.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa