Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Makambako, Bi. Amina Kassim katika maadhimisho ya wiki ya msaada kisheria,yaliyofanyika leo,katika kata ya Lyamkena,kupitia Shirika la TULILUMWI MAKAMBAKO,ambalo linajishughulisha na utoaji wa msaada wa kisheria katika halmashauri ya Mji Makambako.
Bi, Amina ambaye pia ni Mwanasheria wa halmashauri ya Mji Makambako, amesema kuwa,Jinai ni kitendo chochote kinachofanywa na mtu ambacho ni kinyume na sheria za Nchi na haki za binadamu,kwani huhatarisha usalama wa mtu na Mali zake,pia jinai ipo katika jamii zetu na tunaishi nayo,kwani jinai sio lazima iwe mauaji bali hata wizi wa kuku ni kosa la jinai kwasababu ni kinyume cha sheria za Nchi.
“Kuiba kuku pia ni jinai kwa sababu ni kinyume cha sheria za Nchi, Ulawiti, Ubakaji, Mauaji na vitendo vingine vinavyohatarisha usalama wa watu pia ni jinai na hukumu yake ni kifungo gerezani,na katika kila jamii jinai ipo na tunaishi nayo majumbani mwetu kwani wabakaji,wezi,wanaolawiti na wauaji wanatoka katika familia ama jamii zetu tunazoishi”,alisema Bi. Amina.
Ametoa wito kwa wananchi wote kuepukana na matendo ya jinai kwani kujua au kutokujua kuwa jambo Fulani ni kosa au sio kosa kisheria sio kinga dhidi ya sheria, bali mtu ataonekana hana hatia baada ya uchunguzi kufanyika na akithibitika ana hatia atapewa adhabu kwa mujibu wa sheria.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii katika halmashauri ya Mji Makambako,Masinde Ramadhan Masinde amesema kuwa,wakazi wengi wa Mji wa Makambako ni wasiri kutoa taarifa za ukatili zinazofanywa na watu wao wa karibu,na kusababisha ukatili kuongezeka kwani wengi wanaojihusisha na masuala ya ukatili walishafanyiwa ukatili mwanzo.
“Imekuwa ngumu sana kwa wazazi na walezi kutoa taarifa za ukatili wanaofanyiwa wao ama watoto wao,endapo aliyefanya ukatili huo ni mmoja wa familia ama ni mtu wa karibu na familia,kwa kigezo cha kuficha aibu pasipo kutambua kuwa usiri huo una madhara makubwa sana,kwani aliyefanyiwa ukatili huweka kisasi dhidi ya mtu aliyemfanyia ukatili na kuamua kulipiza kwa wengine”, alisema Bw. Masinde.
Bw. Masinde ametoa wito kwa wananchi wote kutoa taarifa juu ya vitendo vya kikatili vinavyofanyika katika familia na jamii zao,na kutomaliza masuala ya ukatili na migogoro ya ndoa,mirathi na mambo mengineyo kama ubakaji na ulawiti kifamilia bali kisheria,ili kuepuka athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza, lakini pia kutenga muda wa kukaa na watoto wao ili kutambua hisia zao juu ya maisha yao ya shule na mitaani na kuwasikiliza.
“Wasikilizeni watoto wenu wanapokataa kusoma shule Fulani,kuna kuwa na sababu zinazomfanya mtoto akatae na siyo kumlazimisha kusoma shule hiyo kisa umelipa ada uliyoipata kwa shida,wasikilize watoto na jengeni urafiki na watoto wenu ili waweze kuwaambia mambo yanayowatatiza shuleni,kwani wanakutana na changamoto nyingi na wazazi mnachojali kulipa ada tu,endapo mtoto atakataa ama kwenda shule au kwa ndugu Fulani asikilizwe kwani wengine wanafanyiwa vitendo vya kikatili na watu hao,”, alisema Masinde.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Msaada Kisheria kitaifa kwa mwaka huu ni “MABORESHO ENDELEVU YA HAKI YA JINAI,KUIMARISHA UPATIKANAJI HAKI JINAI KWA WAKATI”.
MWISHO.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa