Na. Lina Sanga
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Kenneth Haule amewataka wananchi wa Mtaa wa Sekondari Kata ya Maguvani,kuitumia fursa ya mradi wa urasimishaji ardhi unaotekelezwa na MKURABITA kupitia Ofisi ya Rais ikulu ya Upangaji na Upimaji ardhi bura na kuandaa hati miliki kwa gharama nafuu ambazo zinaandaliwa katika ofisi za mtaa huo na kukabidhiwa na wananchi,ili kumpunguzia mwananchi mzigo wa kulipia gharama kubwa na kutumia muda mrefu kufuatilia hati.
Haule ametoa wito huo jana wakati akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Sekondari uliopo Kata ya Maguvani ambao umefikiwa na mradi huo wa upangaji na upimaji ardhi na kukabidhiwa hati kwa gharama nafuu.
Amesema kuwa Serikali inawajali wananchi wa halk ya chini na kuamua kuratibu mpango wa urasimishaji ardhi kwa gharama nafuu Nchini ili hata mwananchi wa hali ya Chini apimiwe ardhi yake na kukabidhiwa hati miliki kwa kulipia hati pekee na sio zoezi la upangaji na upimaji ardhi,lakini bado mwitikio wa wananchi wa mtaa huo ni mdogo na hauridhishi.
"Ndugu zangu Serikali yetu inawajali sana wananchi wa hali ya chini,na imeamua kuleta Mradi huu ili kumpunguzia mwananchi gharama za upimaji wa ardhi na hati miliki, hivi sasa Serikali inakipia upangaji na upimaji wa ardhi wa kila mwananchi,wewe ulipimie hati miliki tena kwa gharama isiyozidi laki moja na nusu lakini bado wengine hadi sasa hawajalipia ili mchakato wa kupata hati miliki uanze na wakabidhiwe hati zao, ni jambo la kushangaza sana na linasikitisha sana kwani katika Halmashauri yetu ya Mji Makambako ni Mitaa mingi yenye uhitaji wa mradi huu lakini kati ya mitaa 54 ni mitaa miwili tu inanufaika na bado hamtoi ushirikiano",alisema Haule.
Ametoa rai kwa wananchi wa mtaa wa Sekondari na Mtaa wa Kikula kuhakikisha wanajitoa katika kufanikisha zoezi hilo kiukamilifu ili kuendana na hadhi ya Mji kwani haileti maana nzuri kwa wananchi wengine wenye uhitaji wa fursa hiyo ambao hawajabahatika kuipata kwenye mitaa yao.
Awali akizungumzia kuhusiana na utekelezaji wa zoezi la upimaji na urasimishaji wa ardhi katika Mtaa wa Sekondari, Msimamizi wa zoezi hilo kutoka ofisi ya Rais ikulu, Henry Tarimo amesema kuwa mpaka sasa watu elfu moja wamepimiwa maeneo yao katika Mtaa wa Sekondari,wananchi waliolipia ni 329 huku waliojitokeza kujua gharama zao ni watu 659.
Naye Afisa ardhi mteule katika Halmashauri ya Mji Makambako,Claudia Kipapi amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kwani mpango huo ukipita, gharama za urasimishaji na umilikishaji wa hati zitakua ni kubwa tofauti na sasa.
Mpango wa Serikali wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Halmashauri ya Mji Makambako unatekelezwa katika mitaa miwili ikiwemo Mtaa wa Sekondari uliopo Kata ya Maguvani na Mtaa wa Kikula uliopo Kata ya Makambako,Serikali inamlipia kila mwananchi gharama za upangaji na Upimaji wa ardhi na jukumu la mwananchi ni kulipia gharama za kuandaliwa hati ya kiwanja kwa gharama nafuu kulingana na ukubwa na matumizi ya kiwanja husika.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa