Na. Lina Sanga
Wananchi wameishauri Serikali kuongeza idadi ya polisi Kata, katika kila Kata nchini hasa zenye idadi kubwa ya watu, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa raia.
Ushauri huo ulitolewa jana na wananchi wa Mtaa wa Majengo, katika ziara ya mbunge wa jimbo la Makambako, Mhe. Deo Kasenyenda Sanga katika Kata ya Majengo.
Imeelezwa kuwa,matukio ya ukatili wa kijinsia yamekuwa yakitendeka kama ubakaji wa wanawake wazee,na ni ngumu kwa askari Kata mmoja kufika kwa wakati eneo la tukio kwani Kata ni kubwa sana.
Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilimahewa,Antony Ngollo ameliomba Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kukamilisha uwekaji wa huduma ya umeme kwa takribani nyumba 400 zilizokosa huduma hiyo katika Mtaa wa Kilimahewa ili wananchi hao wanufaike na huduma hiyo.
Mhe. Deo Sanga,Mbunge wa jimbo la Makambako ametoa ahadi kwa wakazi waliokosa umeme katika Mtaa wa Kilimahewa kuwa atalishughulikia kwa kushirikiana na Meneja wa TANESCO Makambako ili vifaa vinavyohitajika kukamilisha mradi huo vipatikane na wananchi wapate huduma ya Umeme.
Kaimu Meneja wa TANESCO Makambako,Ezekia Sambala amesema kuwa wakati wa utekelezaji wa mradi Mtaa wa Kilimahewa mwaka wa fedha 2022/2023 mradi ulishindwa kukamilika kutokana na ukosefu wa vifaa ambavyo vinatarajiwa kununuliwa katika mwaka huu wa fedha 2023/2024.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa