Na. Lina Sanga
Wanufaika wa TASAF katika Mkoa wa Njombe wametakiwa kuupokea mradi wa parachichi ulioanzishwa kwa ajili ya kuwawezesha kuwa na kipato endelevu na kuacha uoga wa kuboresha maisha yao kwa hofu ya kutolewa TASAF.
Wito huo umetolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kabla ya kugawa miche ya parachichi kwa wanufaika wa TASAF,Halmashauri ya Mji Makambako.
Mhe. Ndejembi amesema kuwa, Mradi wa TASAF uliopo sasa ulikuwa unaisha mwaka huu lakini jitihada za Mhe. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania muda wa utekelezaji wa mradi huo umeongezeka hadi mwaka 2025.
Amesema kuwa,ipo haja ya wanufaika wa TASAF kutambua kuwa lengo kuu la TASAF ni kuboresha maisha na kutokomeza umasikini,na baada ya muda Fulani ni lazima walionufaika waondolewe na kuingizwa wanufaika wapya ,lakini pia kuna kuisha kwa miradi ya TASAF hivyo hawana budi kuwa tayari kuendeleza miradi wanayopewa na kuboresha kipato chao.
Ameongeza kuwa,baadhi ya wanufaika wanadanganywa kuwa endapo watapanda parachichi watatolewa kwenye mpango wa TASAF,na wapo baadhi wanaibua vikwazo kwa kusingizia ukosefu wa mbolea na mahitaji mengine kutokana na uwoga wa kutolewa TASAF.
“Wanufaika wa TASAF acheni uoga wa kuboresha maisha yenu kwa kuhofia mtatolewa TASAF,hata ukipanda parachichi leo hutatolewa hadi kipato chako kitakapo boresheka,na mkumbuke kuwa nimewaambia mwaka 2025 mradi huu wa TASAF unaisha na wote mnatolewa,TASAF kwa mwaka unapata laki moja na elfu themanini,lakini mti wa parachichi baada ya miaka mitatu kila mti mmoja utakupa si chini ya laki mbili,narudia acheni uoga pandeni parachichi”,alisema Mhe. Ndejembi.
Aidha,ametoa pongezi kwa Uongozi wa Halmashauri ya Mji Makambako kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi ndani ya muda,pamoja na ushirikiano wa idara na idara katika utekelezaji wa miradi wa pamoja na kumuagiza Mkurugenzi wa TASAF kumuandikia barua ya pongezi Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako,Bi. Neema Chaula kwa usimamizi bora wa miradi.
Ametoa rai kwa watumishi wote kuwajibika kwa kutambua dhamana walizonazo na kutimiza wajibu,kushirikiana katika kutekeleza majukumu ,kufuata sheria,taratibu,kanuni na miongozo mbalimbali ya taaluma zao na ajira kwa ujumla na kutofanya kazi kwa mazoea.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa