Na. Lina Sanga
Kamati ya fedha na uongozi ya Halmashauri ya Mji makambako imewataka watumishi kutunza nyumba wanazoishi ambazo zimejengwa na Serikali kwa kuzithamini kama za kwao na kufanya marekebisho madogo madogo inapobidi ili nyumba hizo zidumu muda mrefu.
Kamati ya fedha na Uongozi imetoa rai hiyo leo katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha kuishia robo ya kwanza(Julai- Septemba) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika Kata ya Kitisi,Kitandililo na Mahongole.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uongozi Mhe. Hanana Mfikwa akizungumza na watumishi wawili wa Zahanati ya Kijiji cha Ibatu,ambao wataishi katika nyumba mpya pacha iliyojengwa kupitia mfuko wa kunusuru kaya masikini (TASAF) pamoja na wananchi, amewataka watumishi wote wanaokabidhiwa nyumba za Serikali kwa ajili ya kuishi kuhakikisha wanazitunza kwani nyumba hizo ni zao hivyo hata kioo kikivunjika kununua kingine ni lazima.
Pia,Mhe. Hanana amewapongeza wananchi wanaoshiriki katika usimamizi na utekelezaji wa miradi katika maeneo yao kwa niaba ya Serikali,kwa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kukamilika katika ubora unaoendana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Lakini pia,amewataka mafundi wakuu wanaotekeleza miradi ya Serikali kuhakikisha wanawalipa mafundi wanaowasaidia kazi kama vibarua kwa wakati ,ili kuepuka migogoro isiyokuwa na ulazima na kuhakikisha wanakamilisha miradi ndani ya muda uliopangwa kwa viwango na ubora unaokubalika.
Ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha watoto wote wanapata mahitaji muhimu kwa ajili ya ustawi wa watoto ikiwa ni pamoja na kupata chakula shuleni, na kuwataka wananchi wa Kijiji cha Usetule kujitoa kusafisha mazingira ya shule ya msingi shikizi ya Magomati kwa kung’oa visiki ili iwe rahisi kwa Wakala wa barabara Mijini na Vijijini(TARURA) kutengeneza barabara za kudumu.
Kamati ya fedha na uongozi leo imefanya ziara na kukagua miradi minne ambayo ni pamoja na kukagua miundombinu ya nyumba pacha ya Walimu shule ya sekondari Kitisi,ujenzi wa shule mpya ya sekondari Mbugani katika Kata ya Kitandililo,ujenzi wa nyumba pacha ya watumishi katika Zahanati ya Ibatu na Ujenzi wa madarasa sita na matundu 12 ya vyoo shule ya msingi shikizi Magomati.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa