Na. Lina Sanga
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha,Mhe. Hanana Mfikwa ametoa rai kwa wazazi kushirikiana na walimu katika malezi ya wanafunzi,kitaaluma na utunzaji wa miundombinu ya shule.
Mhe. Hanana ametoa rai hiyo leo katika ziara ya kamati ya fedha na uongozi ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Mahongole, ambapo Kamati hiyo ilifanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Manga.
Akizungumza na baadhi ya wazazi ambao ni wajumbe wa kamati za ujenzi wa mradi huo,amewataka kuwashirikisha na wazazi wengine juu ya umuhimu wa wazazi kushirikiana na walimu katika malezi ya watoto wanapokuwa shuleni na hasa namna ya utunzaji wa miundombinu ya madarasa ili yatumike kwa muda mrefu.
Amesema kuwa ipo haja kwa wazazi kufidia gharama ya kurekebisha miundombinu ya madarasa na hata madawati endapo watoto wao wameharibu,kwani kwa kufanya hivyo madarasa hayo yatatumika muda mrefu badala ya kusubiri Serikali ifanye matengenezo ambayo huenda ikachukua muda mrefu kutekelezeka.
"Niwaombe wazazi wenzangu mtoto anapovunja kioo au kuvunja dawati au kuharibu kitu chochote,gharama ijulikane na wazazi wachangie na maisha yaendelee,kwani hata nyumbani kwako ukivunja chupa ya chai unanunua nyingine kwa sababu kuna kuvunja bahati mbaya,hawa watoto wakivunja kioo wasiadhibiwe mana adhabu haifanyi kioo kuwa kizima badala yake wazazi wachangie na kuwaelimisha watoto juu ya uharibifu waliofanya",alisema Mhe. Hanana.
Aidha,ameipongeza Kamati ya Usimamizi na Ufuatiliaji wa miradi ya Halmashauri ya Mji Makambako,kwa usimamizi mzuri wa miradi pamoja na kamati za ujenzi za wananchi wa eneo husika kwa kujitoa katika usimamizi wa miradi hadi inapokamilika.
Kamati ya fedha na Uongozi leo imetembelea miradi minne ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Manga, Mawande, Ikwete na shule ya Msingi Makambako,shule hizo zote zilipokea fedha kiasi cha mil. 45 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa