Na. Lina Sanga
Wilaya ya Njombe kupitia Halmashauri zilizopo chini ya Wilaya hiyo imekusudia kukusanya mapato kwenye vyanzo vya ndani kwa asilimia 100 ifikapo juni,2023 na kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025,kwa kipindi cha nusu mwaka kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo,kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Mhe. Kissa amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Wilaya ya Njombe imekusudia kukusanya Bil. 13.12 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani vilivyopo kwenye Halmashauri tatu zilizo chini ya Wilaya ya Njombe, ambapo Bil. 5.7 kukusanywa katika vyanzo vya ndani vya mapato katika Halmashauri ya Mji Njombe,Bil. 3.7 kukusanywa katika vyanzo vya ndani vya mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Bil. 3.5 kukusanywa katika vyanzo vya ndani vya mapato katika Halmashauri ya Mji Makambako.
Amesema kuwa, hadi kufikia desemba 31,2022 Wilaya ya Njombe imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani Bil. 5.93 sawa na asilimia 45.3 ya lengo ambapo katika Halmashauri ya Mji Njombe jumla ya Bil. 2.98,Halmashauri ya Mji Makambako imekusanya Bil. 1.49 na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni Bil. 1.46.
Aidha amebainisha Wilaya hiyo imefanikiwa kutoa mikopo ya asilimia 10 ka Vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri,ambapo jumla ya Mil. 957.3 zimetolewa kwa vikundi 106 vya wanawake na vijana na 24 kwa watu wenye ulemavu.
Ameongeza kuwa,Wilaya ya Njombe imeendelea kutekeleza miradi miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri zake, ambapo kwa kipindi cha julai hadi desemba 2022,Wilaya ya Njombe imetekeleza miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 62 kwa ajili ya kidato cha kwanza kwa mwaka 2023,yenye thamani ya Bil. 1.24 ambapo katika Halmashauri ya Mji Njombe jumla ya madarasa 26 yenye thamani ya Mil. 520 yalijengwa na yanatumiaka,Halmashauri ya Mji Makambako jumla ya madarasa 21 yenye thamani ya Mil. 420 yamejengwa na yanatumika na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe madarasa 15 yenye thamani ya Mil. 300 yamejengwa na yanatumiaka.
Pia ameongeza kuwa, Wilaya ya Njombe imepokea Bil. 1.4 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya tatu za Sekondari za wasichana ,ambapo Halmashauri ya Mji Njombe imepokea jumla ya Mil. 470,Halmashauri ya Mji Makambako imepokea jumla ya Mil. 470 na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Imepokea jumla ya Mil. 470.
Ametoa shukurani kwa Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya elimu pamoja kuongeza bajeti ya Wakala wa barabara Vijijini na Mijini (TARURA) ,kwani kupitia ongezeko hilo matengenezo ya barabara yanafanyika kwa wakati na kupunguza kero kwa wananchi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa