#Repost from Idara ya Habari- Maelezo
#Mwaka 2023 ni mwaka uliokuwa na neema na changamoto zake kwetu kama nchi. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuumaliza mwaka tukiwa na umoja na mshikamano.
*MAFANIKIO YA NCHI KWA MWAKA 2023*
#Katika suala la Amani, Ulinzi na Usalama wa nchi yetu, ninafarijika kusema kwamba, mipaka yote ya nchi yetu iko salama. Aidha, vikosi vyetu vya ulinzi na usalama vipo imara. Sote tulishuhudia namna vikosi vyetu vilivyojitoa katika uokoaji na kurejesha hali ya kawaida pale tulipopatwa na maafa. Nitumie fursa hii kuvipongeza kwa ujasiri na uzalendo wao.
#Tumeendelea kudhibiti mfumuko wa bei, ambao katika kipindi cha Januari hadi Novemba, 2023 ulipungua hadi wastani wa 3.9%, ikilinganishwa na wastani wa 4.3% kipindi kama hicho mwaka jana. Aidha, ukuaji wa Uchumi na Pato la Taifa kwa mwaka 2023 ulikadiriwa kuongezeka kwa 5.2% ikilinganishwa na 4.7% mwaka jana wa 2022.
#Katika mwaka 2022/23, Serikali ilifanikiwa kupokea kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.3 sawa na shilingi trilioni 3 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, sawa na 100% ya kiasi kilichopangwa kukopwa.
#Deni la Taifa limeendelea kuwa himilivu. Uwiano wake kwa pato la Taifa, kwa thamani ya sasa ni 35.6% ukilinganisha na ukomo wa 50%.
#Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 504 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.6, ikiwa ni ongezeko la 58% ikilinganishwa na miradi 292 iliyosajiliwa mwaka 2022. Kati ya miradi iliyosajiliwa, miradi 55 ilikuwa ni ya upanuzi, hali inayoashiria imani kubwa ya wawekezaji kwenye uchumi wetu na mwenendo wa ukuaji wake.
#Kwa upande wa ukusanyaji wa kodi, kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 2023 ukusanyaji ulifika shilingi trilioni 22.6, ikiwa ni ongezeko la 8% ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2022.
#Tumeongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 751 mwaka jana 2022 hadi shilingi bilioni 970 mwaka huu, sawa na ongezeko la 29%. Shabaha yetu ni kuchochea kiwango cha ukuaji wa sekta ya kilimo kufikia 10% kwa mwaka, ifikapo mwaka 2030.
#Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 17,148,290 msimu wa 2021/2022 hadi tani 20,402,014 msimu wa mwaka 2022/2023, hivyo kufikisha 124% ya kiwango cha utoshelevu wa chakula nchini.
#Aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 116 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) ili kuchochea soko, ambapo katika awamu ya kwanza, NFRA imenunua jumla ya tani 200,293 za mazao.
#Tani 204,818.16 za mbolea zilikuwa zimesambazwa kwa wakulima katika Mikoa yote ya Tanzania Bara, ikiwemo ruzuku ya Serikali yenye thamani ya shilingi bilioni 67.82. Serikali inaendelea kutoa ruzuku ya mbolea, mbegu na viuatilifu kwa baadhi ya mazao ya kimkakati kama vile pamba, korosho, alizeti, chikichi, kahawa na chai.
#Serikali imeendelea na jitihada za kuwaingiza vijana na wanawake kwenye uzalishaji. Mpaka tunamaliza mwaka huu 2023, jumla ya ekari 201,241 zimetengwa kwa shughuli hiyo. Aidha, tumeanzisha programu ya kilimo cha kisasa iitwayo Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ili kuongeza uzalishaji, kuchochea viwanda vya usindikaji, na kutengeneza ajira kwa vijana.
#Serikali itaendelea kuwekeza kwenye skimu za umwagiliaji ili kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 727,000 hadi hekta 822,000 ifikapo Desemba 2024.
#Mwaka huu tumeshuhudia ongezeko la 6.43% la thamani ya madini yaliyozalishwa. Pia, kumekuwa na ongezeko la 5.8% ya madini yaliyouzwa nje ya nchi hadi kufikia dola za Marekani bilioni 3.15.
Kwa kutambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo kwenye sekta hii, mwaka huu, Serikali ilinunua mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji hao.
#Mwelekeo wa Serikali ni kuendelea na ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini hapa nchini, hatua itakayotuwezesha kuongeza thamani na fursa zaidi za ajira.
#Kwa kipindi cha Oktoba 2022 hadi Oktoba 2023, tumepokea watalii 1,750,557 ikilinganishwa na watalii 1,381,881 walioingia kipindi kama hicho mwaka 2022. Katika kipindi hichohicho, mapato kupitia sekta ya utalii yalifikia dola za Kimarekani bilioni 3.22 ikilinganishwa na dola za Kimarekani bilioni 2.33 kipindi kama hicho mwaka 2022.
#Serikali imeendelea na utekelezaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambapo vipande vya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Makutupora vimefikia zaidi ya 90%. Aidha, tumepata udhamini wa Benki ya Maendeleo Afrika utakaowezesha uendelezaji wa kipande cha Tabora-Kigoma na Uvinza-Musongati.
#Nimekuwa nikisikia mabadiliko ya tarehe za kuanza kwa safari za treni. Naelekeza, ifikapo mwisho wa mwezi Julai 2024, safari kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma zianze
#Kwa kipindi cha takriban miezi minne ya mwaka huu wa 2023, nchi yetu imekumbwa na upungufu wa umeme, uliosababisha mgao. Panapo majaliwa, mwezi Februari 2024 tutawasha rasmi mtambo wa kwanza na mwezi Machi tutawasha mtambo wa pili katika Mradi wa JNHPP. Mitambo ambayo itatupatia jumla ya Megawati 470 na hivyo kufidia upungufu wa sasa ambao ni Megawati 300 tu.
#Hatua ya kuwasha mitambo miwili ya JNHPP, itakwenda sambamba na kuwasha mtambo wa Rusumo utakaoongeza Megawati 27.
#Kufikia mwezi Novemba, 2023, Serikali ilikuwa imepeleka umeme katika vijiji 11,447 sawa na 93% ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara. Kazi ya usambazaji wa umeme vitongojini nayo inaendelea.
#Mwaka 2023, Serikali imeajiri jumla ya wataalam 17,309 na ilitenga jumla ya shilingi bilioni 190.9 kwa ajili ya kununua dawa.
#Serikali imeweka MRI 5 na CT – Scan 30 kati ya 32 katika vituo vya kutolea huduma katika Mikoa 24 kati ya 26. Imesambaza seti 123 za vifaa vya huduma kwa watoto wachanga na wenye uzito pungufu, na mashine 125 za ultra sound. Vilevile, imetoa mashine 140 za kutibu dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama. Aidha, imesambaza magari 369 ya kubebea wagonjwa na uratibu wa huduma za afya kote nchini.
#Kwa upande wa Matibabu ya Kuchuja Damu kwa Wagonjwa Sugu wa Figo yaani Dialysis, Hospital 11 za Rufaa za Mikoa zinatoa huduma.
#Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya maji uliotuwezesha kukamilisha miradi 506 ikiwemo 436 ya vijijini na 70 ya mijini yenye uwezo wa kuhudumia wananchi 5,754,340 na kuongeza wastani wa upatikanaji wa huduma za maji hadi 88% mijini na 77% vijijini.
#Aidha, Serikali imepata dola za Marekani milioni 600 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji kutoka ziwa Victoria hadi Dodoma.
#Mwaka 2024, Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 48 kwa ajili ya kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi 8,000 wa stashahada (diploma) kwa fani za kipaumbele.
#Kiasi cha shilingi bilioni 2.94 kilitumika kuwafadhili wanafunzi 636 kwenye masomo ya sayansi katika vyuo mbalimbali kupitia Samia Scholarship kwa mwaka 2022, mwaka huu, Serikali imetenga shilingi bilioni 6.7 ambayo hadi sasa inawafadhili wanafunzi 1,019.
#Kutokana na kuimarika kwa ushirikiano wetu na Mataifa na mashirika mbalimbali, kupitia ziara zimetuwezesha kupata kiasi cha dola za Kimarekani milioni 550 kwa ajili ya miradi ya usalama wa chakula, tumepata dola za Marekani milioni 297.64 kwa ajili ya mradi wa mawasiliano vijijini.
#Tumenufaika na Chuo cha Teknolojia cha IIT Madras kutoka India ambacho kimefungua Kampasi Zanzibar, tumepata soko la mabondo ya samaki, parachichi, kahawa, soya n.k, vilevile, tumepata nafasi za kazi 500 kwa wauguzi wetu kutoka nchini Saudi Arabia.
#Baada ya takribani miaka sita, tumerejeshwa kwenye Mfumo wa Changamoto za Milenia (MCC) wa
Marekani, ambapo utekelezaji utaanza mwakani.Kutokana na mwenendo wetu mzuri kwenye uchumi, mwezi huu tumepokea kutoka Benki ya Dunia dola za Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya kusaidia bajeti ya Serikali.
#Katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi mwaka huu (COP28), Tanzania iliahidiwa na Jumuiya ya Kimataifa chini ya Uongozi wa Global Centre on Adaptation na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 9.9 kwa ajili ya miradi itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
#Katika Mkutano wa nane wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia, jumla ya dola milioni 53 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya mazingira na maendeleo Tanzania.
#Mwaka wa 2024, Programu ya matumizi ya nishati safi inayolenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa Barani Afrika itawekewa mfumo rasmi wa kuifanya iwe endelevu na yenye manufaa. Programu hiyo itatusaidia pia kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo la kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.
#Natumia fursa hii kuzipongeza timu zote zilizofanya vyema na wanamichezo wote waliofanya vizuri mwaka huu. Ahadi yetu ni kuendelea kuwekeza kwenye michezo hususan kwa vijana, kwani michezo ni ajira pia. Hivyo, tutahakikisha tunaendelea kulea vipaji kuanzia ngazi za shule kwa kuhakikisha michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA inaendela kufanyika.
#Nawashukuru wadau wa siasa kwa kuweka maslahi ya nchi mbele na niwaahidi kwamba, tutaendelea kushirikiana nao. Kwa upande mwingine, tumeendelea kushuhudia vyama vyote vya kisiasa vikitekeleza shughuli zao kwa uhuru na uwazi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
*MATARAJIO YA NCHI KWA MWAKA 2024*
#Tunaadhimisha miaka 60 ya Muungano na miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Matukio haya muhimu kwa Taifa letu ni chachu ya kuendelea kudumisha umoja wa Kitaifa na kuimarisha ustawi wa jamii yetu.
#Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni tukio jingine tunalolitarajia mwakani kwa tarehe itakayotangazwa na Mamlaka husika. Nitoe rai kwa Watanzania kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo, ili tuchague viongozi wanaotufaa.
#Tutaendelea kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuhakikisha usalama wa chakula. Tutaendelea kutekeleza programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT). Aidha, tutaanza kutekeleza miradi ya kuuza na kukodisha kwa bei ya ruzuku zana za kilimo kwa wakulima ikiwamo matrekta.
#Vile vile tutaendelea pia na mageuzi (reforms) katika sekta mbalimbali, ikiwemo uendeshaji wa mashirika ya umma na taasisi, lengo likiwa kuongeza ufanisi na tija katika uendeshaji wake. Tutaimarisha pia utekelezaji wa Sera ya Elimu ili kuhakikisha kuwa tunaanda watoto wetu kwa mazingira ya sasa. Vilevile, tutaendelea na mchakato wa kuandika Dira Mpya ya Maendeleo.
#Kwa mujibu wa sheria tutaboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Natoa wito kwa wote wenye sifa wajitokeze pindi zoezi hilo litakapotangazwa na Mamlaka husika.
#Serikali itaendelea kushirikiana zaidi na taasisi tanzu za Kampuni Changa na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wake. Aidha, pamoja na mikutano mingine, tutakuwa wenyeji wa Kilele cha Nchi 25 za Afrika zinazozalisha Kahawa.
#Katika kuendelea kujenga uhimilivu na uwezo wetu wa kukabiliana na majanga, ikiwemo majanga ya moto, Serikali itachukua hatua za kulijengea uwezo zaidi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na taasisi nyingine zinazoshirikiana nazo ili kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga ikiwemo majanga ya moto.
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - Maelezo*
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa